2013-03-06 12:09:43

Papa anawashukuru Makardinali kwa upendo, umoja na mshikamano wa kidugu waliomwonesha!


Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita ni mtu ambaye anaguswa na matukio mbali mbali yanayomzunguka na pia ni mtu wa shukrani, hata kwa mambo ya kawaida wanayomtendea ndugu zake katika Kristo. Ni maneno ya Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican alipokuwa anaelezea jinsi ambavyo Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alivyopokea ujumbe wa simu ya maandishi kutoka kwa Makardinali kama alama ya shukrani kwa utume wake kwa Kanisa katika kipindi cha miaka minane, aliyojitoa bila ya kujibakiza kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Padre Lombardi anasema, ujumbe waliomwandikia ni mfupi, lakini unaoonesha ule ushuhuda wa upendo na mshikamano wa kidugu pamoja na uwepo wake endelevu katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya maisha ya kiroho yanayofumbatwa katika sala na tafakari ya kina. Idadi kubwa ya Makardinali wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura ni wale walioteuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika kipindi cha miaka minane ya uongozi wake.

Kwa hakika, anasema Padre Federico Lombardi, Baba Mtakatifu mstaafu amewashukuru Makardinali kwa kumwonesha upendo na mshikamano wa kidugu katika kulitumikia Kanisa la Kristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.