Licha ya kasoro ndogo ndogo, wananchi wa Kenya kwa ujumla wameonesha ukomavu wa kidemokrasia!
Askofu Martin Kivuva wa Jimbo Katoliki Machakosi, anawashukuru na kuwapongeza wananchi
wa Kenya kutokana na uvumilivu na uzalendo waliouonesha wakati wa mchakato mzima wa
uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Kenya, hapo tarehe 4 Machi 2013. Kimsingi kumekuwepo
na hali ya utulivu licha ya matukio kadhaa ya uvunjifu wa amani yaliyopelekea watu
17 kupoteza maisha yao mjini Mombasa.
Askofu Kivuva anasema, wananchi wengi
wamejitokeza kushiriki katika uchaguzi mkuu nchini humo. Makosa katika daftari la
wapiga kura ni jambo la kawaida linaloweza kurekebishwa kwa ajili ya mafao ya maendeleo
ya wananchi wa Kenya kwa siku za usoni.
Ni matumaini ya Askofu Kivuva kwamba,
amani na utulivu vitaendelea kutawala nchini humo ili kujenga na kuimarisha utawala
bora unaozingatia mafao ya wengi. Kwa mara ya kwanza wananchi wa Kenya wamepiga kura
kwa kutumia Katiba Mpya iliyopitishwa kunako mwaka 2010.