Askofu mkuu Boniface Lele wa Jimbo kuu la Mombasa hivi karibuni aliwataka waamini
na wananchi wa Kenya kwa ujumla kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda na kudumisha
misingi ya haki, amani na utulivu; kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu.
Wahakikishe
kwamba, wanachagua viongozi bora watakaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi
na maendeleo ya wananchi wote wa Kenya bila kujikita katika ukabila, udini na umajimbo,
kwani haya ni kati ya mambo yanayoweza kukwamisha mchakato wa mageuzi ya kidemokrasia
na maendeleo ya wengi. Ni changamoto kwa wananchi wa Kenya kukubali na kuwaheshimu
wale watakaoshinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatatu, tarehe 4 Machi 2013
kama kielelezo cha utashi wa wananchi wa Kenya.
Pale ambapo haki haikuzingatiwa,
wahusika waitafute haki hii kwa njia za kisheria na wala wasiwatumbukize wananchi
katika vurugu na kinzani zisizokuwa na tija wala maendeleo kwa Wakenya. Watu wanasubiri
kuona Kenya inayoendelea kusimikwa katika misingi ya amani na umoja wa kitaifa. Mafao
ya wananchi wa Kenya hayana budi kupewa kipaumbele cha kwanza, kuliko kitu kingine
chochote kile!
Hata katika uchaguzi mkuu wa Mwaka 2013 bado kuna damu ya watu
wasiokuwa na hatia imeendelea kumwagika nchini Kenya. Amani na utulivu ni jambo la
muhimu sana wakati huu Tume ya Uchaguzi inapoendelea kuhesabu kura kwa njia za kisasa
zaidi ili kuongeza kasi ya kuhesabu kura kwa kuzingatia kanuni za ukweli na uwazi,
ili kuondoa dhana ya wizi wa kura ambao umekuwa ni wimbo usiokuwa na msikilizaji mara
baada ya chaguzi nyingi Barani Afrika.
Taarifa zinabainisha kwamba, wananchi
waliojitokeza kupiga kura ni sawa na asilimia 70% ya Wakenya millioni 14.3 waliokuwa
wanatarajiwa kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu uliomalizika.