2013-03-05 07:46:27

Msimwekee Roho Mtakatifu vizingiti!


Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, akizungumza na Radio Vatican anabainisha kwamba, hiki ni kipindi muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa. RealAudioMP3

Katika siku chache zijazo, Makardinali watapiga kura ya kumchagua Khalifa Mpya wa Mtakatifu Petro baada ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kun’atuka kutoka madarakani.

Kardinali Pengo anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali ili kumwomba Roho Mtakatifu aweze kulipatia Kanisa mchungaji mkuu kadiri ya mpango wake. Anaonya kwamba, kuna baadhi ya watu wanaotaka kumwekea Roho Mtakatifu masharti katika mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya. Kardinali Pengo anasema upepo huvuma unakopenda, sauti yake husika, lakini hauonekani. Anawaalika waamini kumwachia Roho Mtakatifu aweze kutekeleza kazi yake! Hii ndiyo imani ya Kanisa Katoliki.

Kardinali Polycarp Pengo ambaye pia ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam anasema, hali ya amani na usalama nchini Tanzania bado ni tete. Anawaalika waamini kuzidi kujiweka mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Moyo wa kutaka kulipiza kisasi si wa Kikristo na kwa namna ya pekee anasema Kardinali Pengo si wa Kikatoliki. Kamwe waamini hata baada ya kudhulumiwa wasitake kulipiza kisasi, bali yote wamwachie Mwenyezi Mungu!

Kuhusu uhusiano kati ya Waislamu na Wakristo nchini Tanzania, Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania katika hotuba yake ya Mwisho wa Mwezi Februari 2013 alikuwa na haya ya kusema:


Ndugu wananchi;

Jambo la pili ninalopanga kulizungumzia siku ya leo ni uhusiano wa Wakristo na Waislamu hapa nchini. Kwa miezi kadhaa sasa tangu mwaka wa jana kumekuwepo na matukio kadhaa yanayosababisha mifarakano na kupandikiza chuki baina ya waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu. Matukio ya kauli na vitendo vya kudharau dini za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu vya dini hizo, kuchoma moto nyumba za ibada na mzozo kuhusu nani achinje. Kumekuwepo na matumizi mabaya ya radio na simu za mkononi na mifumo mingine ya mawasiliano iliyoeneza maneno na ujumbe wa chuki na vitisho kwa waumini na viongozi wa dini zetu hizi kubwa hapa nchini. Kauli na matendo hayo, katika baadhi ya maeneo yamekuwa chanzo cha uhasama na magomvi baina ya waumini na hatimaye kusababisha vifo kama ilivyotokea Buseresere Mkoani Geita na Beit-el-Ras, Zanzibar.

Ndugu zangu;

Watanzania hatujawahi kuwa hivi, kumetokea nini? Miaka yote Watanzania ni watu tunaotambua na kuheshimu tofauti za dini zetu mbalimbali tunazoabudu. Watanzania ni waelewa na kwa ajili hiyo tumekuwa tunavumiliana kwa tofauti zetu na ndiyo maana tumekuwa tunaishi pamoja kidugu, kwa umoja na kushirikiana kwa mambo yote yanayotuhusu maishani isipokuwa wakati kila mmoja anapoingia kwenye nyumba ya ibada kumuomba Mola kwa misingi na taratibu ya dini yake.

Watanzania wa dini zote na makabila tofauti wanaishi nyumba moja, wanasoma pamoja, wanafanya kazi pamoja kwa udugu, upendo, umoja na ushirikiano. Kuna koo na familia zenye watu wa dini tofauti, wengine Waislamu na wengine Wakristo. Wapo Waislamu na Wakristo wameoana, wamezaa na wamejukuu na kila mmoja amebakia kuwa mfuasi wa dini yake. Wapo pia ambao hawakuoa lakini wamezaa watoto na wanashirikiana kulea watoto wao. Hayo ndiyo maisha ya Watanzania na hiyo ndiyo Tanzania yenye amani na utulivu tuliyozaliwa, kukua na kuishi. Nawasihi sana Watanzania wenzangu, tuienzi na kuidumisha tunu hii waliyotujengea mababu zetu.

Ndugu Wananchi;

Kuna wenzetu kwa sababu wanazozijua wao na kwa manufaa wanayoyajua wao wanataka kutuvurugia nchi yetu hii nzuri. Tusiwape nafasi wachochezi hawa kwani hawatutakii mema na wala hawazitakii mema dini zetu na nchi yetu. Sisi katika Serikali hatutasita kuwachukulia hatua wale wote wanaochochea chuki za kidini, wanaodharau vitabu vitakatifu vya dini nyingine na wanaokejeli dini nyingine.

Nimewakumbusha Polisi na mamlaka husika kote nchini wasifanye ajizi kwenye matukio ya namna hiyo. Wawachukulie hatua stahiki wale wote wanaohusika. Nimewataka wazingatie msemo wa Kiswahili usemao “ajizi nyumba ya njaa”. Wachochezi wa mifarakano na chuki za kidini wasipodhibitiwa ipasavyo wataleta maafa kwa Watanzania wasiokuwa na hatia. Nimewakumbusha Wakuu wa Wilaya na Mikoa kama walinzi wa amani wa maeneo yao ya uongozi, watimize ipasavyo wajibu wao. Pia nimewataka Polisi wakamilishe mapema upelelezi wa makosa ya vurugu za kidini na wahusika wafikishwe haraka kwenye vyombo vya sheria ili iwe fundisho kwa wengine.

Ndugu Wananchi;

Naendelea kuwasiliana na viongozi wa dini kuzungumza nao juu ya wajibu wao maalum wa kuhakikisha kuwa wafuasi wao hawawi chanzo au sehemu ya tatizo na mifarakano miongoni mwa waumini wa dini mbalimbali nchini. Hali kadhalika naitumia nafasi hiyo kuwakumbusha umuhimu wa kuzungumza na wenzao wa upande mwingine kutatua tofauti au matatizo yanayoathiri uhusiano mwema baina yao.


Ndugu Wananchi;

Kuna msemo maarufu usemao “mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi”. Naomba tuwe wajenga nchi na kamwe tusikubali kuwa wabomoa nchi. Hivi tukiibomoa nchi yetu tutakwenda wapi? Tutaishi wapi? Tusikubali kugeuka wakimbizi ndani ya nchi au nje ya nchi yetu.

Kwa mara nyingine tena, napenda kutumia nafasi hii kuwapa mkono wa pole makanisa, familia, ndugu na jamaa wote wa Mchungaji Kachila na Padri Mushi. Sote tunafahamu machungu waliyonayo kwa kuondokewa na wapendwa wao. Serikali na wapenda amani wote nchini wapo pamoja nanyi katika kipindi hiki kugumu. Vile vile natoa rambirambi zangu nyingi kwa waumini wote wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God na Kanisa Katoliki Tanzania kwa kuondolewa ghafla na viongozi wao. Tuzidi kumwomba Mwenyezi Mungu azipumzishe kwa amani roho za viongozi wetu. Amin.










All the contents on this site are copyrighted ©.