2013-03-05 07:31:47

Haki msingi za binadamu zinalenga mafao ya wengi


Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa wa Vatican, hivi karibuni alishiriki katika kikao cha ishirini na mbili cha Baraza la Haki Msingi za Binadamu, kama sehemu ya maadhimisho ya Miaka 20 tangu Jumuiya ya Kimataifa ilipokutana mjini Vienna kunako mwaka 1993 na kutangaza haki msingi za binadamu zinazofumbata pamoja na mambo mengine haki za kiraia, kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni ambazo zimeendelea kukabiliana na vikwazo vingi katika utekelezaji wake.

Vikwazo hivi vinajionesha kwa namna ya pekee katika huduma duni zinazojionesha katika sekta ya elimu, afya, huduma ya maji safi na salama, chakula na lishe, ukosefu wa usalama, huduma hafifu kwa wahamiaji na wakimbizi, ukosefu wa uhuru wa kuabudu sanjari na uhuru wa kidini. Haya yote ni maeneo nyeti yanayopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa, kama sehemu ya utekelezaji wa haki msingi za binadamu.

Askofu mkuu Mamberti anasema kwamba, mchango wa Baraza la Haki Msingi za Binadamu hauna budi kujikita katika kusimamia na kuratibu mchakato utakaowawezesha watu wengi zaidi kutambua haki na wajibu wao kama njia ya kufikia mafao ya wengi. Ni wajibu wa Baraza hili kuhamasisha watu kuheshimu na kuzingatia haki msingi za binadamu sehemu mbali mbali za dunia na kupinga matumizi ya haki hizi kwa misingi ya kisiasa, bali ziwe ni kwa mafao ya wengi.

Askofu mkuu Mamberti anasikitika kusema kwamba, hivi karibuni kumeikuba kile kinachoitwa “haki mpya za binadamu” zisizozingatia kanuni, maadili na utu wema, hali ambayo imepelekea kinzani na migogoro ndani ya Jamii. Kile kinachodaiwa na watetezi wa haki mpya za binadamu, hakina budi kwanza kabisa kuzingatia mafao ya wengi na ushirikiano wa kimataifa unaodhibitiwa na kanuni auni.

Askofu mkuu Mamberti anabainisha kwamba, kumekuwepo na matukio kadhaa yanayoashiria kuvunjika kwa haki msingi za binadamu kutokana na kutothamini uhuru wa kidini. Jumuiya za Kikristo sehemu mbali mbali za dunia zimeendelea kukabiliana na madhulumu ya kidini, changamoto kwa Serikali husika na Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kidini, kwa kutambua kwamba amani na utulivu ni mambo msingi katika kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu hasa kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu unaowezeshwa na utandawazi pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Ili kudumisha misingi ya haki na amani, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa anasema Askofu mkuu Mamberti, kusimama kidete kulinda na kutetea maisha ya mwanadamu, tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Watoto wana haki ya kuwa na wazazi wa pande zote mbili na kuishi katika familia inayojengeka katika ndoa ya bwana na bibi, ambao kimsingi wanao wajibu wa kuwalea na kuwatunza watoto wao.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kulinda na kutetea haki za watu wenye ulemavu; uhuru wa kidini, uhuru wa kujieleza na kushirikiana na watu wengine ndani ya Jamii pamoja na kupambana na ubaguzi unaofanywa kwa misingi ya jinsia, dini na rangi. Jamii ijenge utamaduni wa kuwaheshimu wanawake badala ya kuwadhalilisha, kuwanyanyasa na kuwadhulumu. Utekelezaji wa haki msingi za binadamu hauna budi kujikita katika kutetea maisha ya mwanadamu.

Mafundisho Jamii ya Kanisa ni mchango mkubwa katika kulinda na kutetea haki msingi za binadamu zinazofumbatwa katika misingi ya kimaadili, asili, utu na heshima ya binadamu. Kila mtu ana haki na wajibu za kutekeleza ndani ya Jamii. Binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa kwa njia ya Damu Azizi ya Kristo. Hii ndiyo sababu msingi inayopelekea Kanisa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu.








All the contents on this site are copyrighted ©.