Mwenyezi Mungu anatambua mateso na kero za watu wake kiasi cha kuamua kuwa ni mwenza
katika hija ya maisha yao!
Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika
na Madagascar, SECAM, Jumapili iliyopita, kwenye Parokia ya Bikira Maria wa Salette,
iliyoko mjini Roma, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea mchakato
wa uchaguzi wa Papa mpya pamoja na kuombea haki, amani na upatanisho Barani Afrika,
lakini kwa namna ya pekee, Tanzania ambayo kwa siku za hivi karibuni imekuwa ni uwanja
wa dhuluma za kidini.
Kardinali Pengo anasema, ustawi na maendeleo ya Kanisa
kwa sasa na kwa siku za usoni, umedhaminishwa kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Makardinali
kutoka sehemu mbali mbali za dunia wamekusanyika mjini Roma kuanza mchakato wa kumchagua
Khalifa wa Mtakatifu Petro, utume ambao Mwenyezi Mungu anawakabidhi binadamu, akitumaini
kwamba, neema yake itawasaidia kutekeleza wajibu huu msingi, ili Mungu aweze kupata
makao miongoni mwa binadamu anayepaswa kuwa kweli ni mdau mkuu katika utekelezaji
wa mipango ya Mungu.
Kanisa ambalo ni Fumbo la Mwili wa Kristo, linashirikiana
kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Khalifa wa Mtakatifu Petro
anayo dhamana kubwa ya kuwaongoza Watu wa Mungu kutekeleza wito wao, kwa kutambua
nafasi na fursa walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu katika kuendeleza historia ya ukombozi
wa mwanadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo ambaye kimsingi ni daraja
kati ya Mungu na mwanadamu.
Kardinali Pengo anabainisha kwamba, Maandiko Matakatifu
yanamwonesha Mwenyezi Mungu anavyoamua kuchukua nafasi ya mwisho katika maisha ya
mwanadamu; kushikamana kwa dhati na maskini, wanyenyekevu wa moyo; wanaodhulumiwa
na kunyimwa haki zao msingi; wanaodhalilishwa na utu wao kutwezwa hata kusukumizwa
pembezoni mwa Jamii.
Ni Mungu anayetambua mateso na kero za watu wake, kiasi
kwamba, anaamua kuwa ni mwenza katika hija ya maisha yao kwa kuwahakikishia kwamba,
kilio cha madhulumu wanayokumbana nayo iko siku kitaweza kusikilizwa; kwani Yeye ni
mwenye haki na wakati utakapowadia atayafanya yote mapya.
Kardinali Pengo anasikitika
kusema kwamba, katika siku za hivi karibuni, Nchi nyingi za Kiafrika zimekuwa ni uwanja
wa madhulumu ya kidini yanayofanywa na baadhi ya waamini wenye misimamo mikali sanjari
na matukio ya kigaidi yanayoendelea kupelekea watu wengi wasiokuwa na hatia kupoteza
maisha yao. Katika matukio kama haya, Wakristo kwa namna ya pekee, wanaalikwa kuisikiliza
ile sauti ya Mungu, ambaye si mwingi wa hasira, bali mpole na mnyenyekevu anayetoa
nafasi kwa kila mtu kutubu na kuongoka, ili aweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani:
haki, amani, upendo na utulivu.
Kanisa kwa kutambua kwamba, linashirikiana
na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya mwanadamu, linapenda kuelimisha,
kuongoza na kuwasaidia watu kujenga dhamiri nyofu inayokumbatia upendo wa dhati, jambo
ambalo ni chukizo kwa waamini wenye misimamo mikali ya kidini na wanaotaka kukumbatia
vitendo vya kigaidi ili kufikia malengo yao!
Amani ni nguvu ya ndani inayoweza
kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya mwanadamu na wala si mtutu wa bunduki:
Haki na amani ni chanda na pete na kikolezo cha maendeleo endelevu yanayowahusisha
binadamu wote pasi wa aina yoyote ile! Umefika wakati kwa watu kujenga utamaduni wa
haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati. Watu wamwongokee Mwenyezi Mungu anayesamehe
na kupenda haki; mambo ambayo yanafumbatwa katika Fumbo la Maisha na Utume wa Kanisa
unaopaswa kushuhudiwa kwa njia ya maisha ya Wakristo. Huu ndio ujumbe maalum wa kipindi
cha Kwaresima.
Khalifa wa Mtakatifu Petro anayekabidhiwa dhamana ya kuliongoza
Kanisa la Kristo anapaswa kwanza kabisa anasema Kardinali Polycarp Pengo kuwa ni Baba
wa Maskini; Mtetezi wa wanyonge na wanaonyimwa na kudhulumiwa haki zao; shahidi makini
wa Fumbo la Mungu lililofumbuliwa na Yesu Kristo katika historia ya maisha ya mwanadamu
yanayofumbata mwanga na vivuli vya giza. Ni kipongozi anayepaswa kuwa mwema na mnyofu
anayetoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao, ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo
na binadamu katika ujumla wao!
Awe ni mfano mwema wa kuigwa kwa maneno na
matendo yanayobubujika kutoka katika kweli za Kiinjili; ambaye yuko tayari kujikana
mwenyewe bna kuubeba Msalaba wake, tayari kumfuasa Yesu, akithubutu hata kuwasamehe
adui zake! Hiki ndicho kielelezo cha maisha ya Kikristo anasema Kardinali Pengo kinachohitaji
toba na wongofu wa ndani.
Kuna haja kwa waamini kujikita katika kutafuta na
kukumbatia yale mambo ya msingi yanayojionesha katika Fumbo la Msalaba wa Kristo,
Mwana wa Mungu. Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha Kanisa; ni mwalimu wa Ukristo
na Upendo wa Kiinjili.
Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa SECAM anahitimisha
mahubiri yake, kwa kumweka Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliyeliongoza
Kanisa kwa kipindi cha miaka minane, chini ya uongozi na usimamizi wa Bikira Maria.
Ni Papa aliyeliongoza Kanisa kwa uaminifu mkubwa, akatumia vyema kipaji chake cha
akili na unyenyekevu. Kwa hakika anastahili kushukuriwa na kupongezwa.
Kardinali
Polycarp Pengo amewaweka pia Makardinali wote wanaoshiriki katika mchakato wa kumchagua
Papa Mpya chini ya uongozi na usimamizi wa Bikira Maria aliyekuwa mwanafunzi mwaminifu
wa Kristo, bila woga, kiasi kwamba, wataweza kuchangia kwa dhati kabisa kumchagua
yule ambaye Mwenyezi Mungu anapenda awe ni Khalifa wa Mtakatifu Petro, msingi wa umoja
wa Kanisa linaloonekana. Umoja katika Mafundisho Tanzu ya Kanisa; katika Imani, Matumaini
na Mapendo. Umoja katika mchakato wa kutafuta haki na amani; umoja kwa kushiriki
taabu na mateso ya wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Umoja uwe ni kielelezo
cha Familia ya binadamu na Muumba wao kwa kujikita katika udugu.