Katika Ukumbi wa Sinodi wa Mjini Vatican , mapema Jumatatu hii , ulianza Mkutano wa
kawaida wa Baraza la Makardinali. Hii ni hatua ya kwanza inayoelekea katika kumchagua
Papa mpya siku za hivi karibuni, uchaguzi unaofanyika katika kikao kinachojulikana
kwa jina la Conclave. Msemaji wa Vatican Padre Federico Lombardi, akizungumza na
wanahabari Jumatatu hii, ametaja idadi ya Makardinali katika kikao cha kwanza, kuwa
142 , ambao 103 ni wapiga kura. Na kwamba Makadinali wengine walikuwa wanatarajiwa
kufika Roma kati ya mchana huu na kesho asubuhi. Kikao cha Makardinali kilianza
na sala ya kuomba Roho Mtakatifu awashukie “Sancte Veni Spiritus". Kardinali Angelo
Sodano, Dekano wa Dekania ya Makardinali alitoa hotuba ya ufunguzi, na alizungumzia
umuhimu wa tukio hili, na kumtaka kila Kardinali kuzingatia kiapo cha kushiriki katika
mkutano huo. Na Kardinali Tarcisio Bertone, ambaye ni msimamizi Mkuu wa kipindi
hiki cha kiti kitupu cha Petro, akijulikana kwa jina la Camerlengo, alimpendekeza,
Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri katika jengo la Kipapa, kutoa tafakari ya neno
wakati wa kuanza kikao cha pili cha adhuhuri kwa siku hii ya Jumatatu. Na Kardinali
Sodano, pia alitoa pendekezo la kupeleka ujumbe kwa Papa Mstaafu Benedikto VXI, na
mapendekezo yote yalikubaliwa. Padre Federico Lombardi na maelezo kwamba, Makardinali
pia katika kipindi cha asubuhi, waliteua wasaidizi watatu wa Camerlengo, kwa mujibu
wa Katiba. Na hivyo walio teuliwa watakuwa wasaidizi kwa musa wa siku tatu. Nao ni
Kardinali Giovani Baptist Re, anayewakilisha Makardinali Maaskofu; Mwingine ni Kardinali
Crescensio Sepe, anayewakilisha Makardinali Mapadre na Kardinali Franc Rodè, anayewakilisha
Makardinali Mashemasi. Baada ya siku tatu kutateuliwa wengine watatu kushika nafasi
hiyo, nao watafanya kwa muda wa siku tatu na mzunguko huo kuendelea hadi kukamilika
kwa mkutano huu. Aidha katika kipindi hiki cha asubuhi , Makardinali 13 walitoa
hotuba zao fupi lakini makini. Na kwamba, kikao kimefanyika katika hali ya udugu na
maelewano na uaminifu wa kusonga mbele.