2013-03-02 08:09:22

Yule mchapakazi katika Shamba la Bwana, sasa ameanza hatua ya mwisho ya hija ya maisha yake hapa duniani! Maajabu makubwa!


Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alikuwa ni mchapakazi katika shamba la Bwana, sasa amegeuka kuwa ni mhujaji anayeanza hatua ya mwisho ya hija ya maisha yake hapa duniani, kwa kujikita katika sala na tafakari kwa ajili ya mafao ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Haya ni maneno ambayo yanatoa mwangwi wake tangu siku ile ya kwanza alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki yapata miaka minane iliyopita!

Miaka minane ya utume uliotukuka, ambao umeshuhudia Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, akijitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Akakumbana na dhoruba kali, kiasi cha kutaka kuliyumbisha Kanisa; lakini kwa ujasiri na busara yake, Mashua ya Mtakatifu Petro ikavuka hata kipindi hiki ambacho wengi walidhani kwamba, eti Yesu anasinzia na wala hakereki kwa yale yaliyokuwa yanatendeka ndani ya Kanisa.

Ni ushuhuda wa Bwana Antonio Pelayo, Balozi wa Hispania mjini Vatican, aliyebahatika kuwa karibu na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika kipindi cha miaka minane ya uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kiongozi mkweli na muwazi ambaye kwake madaraka ni sehemu ya huduma na wala si kitu cha kung'ang'ania sana kama alivyoonesha mwenyewe! Dunia ikapigwa na butwaa! Watu wakaanza kufunga macho! Wanatafuta shuka! Maskini kumbe kumekuchwa!

Huyu ndiye Joseph Ratzinger, aliyechaguliwa na Makardinali kunako mwaka 2005 kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na tarehe 28 Februari kwa utashi na uhuru kamili, akaamua kung'atuka kutoka madarakani; tukio la kihistoria ndani ya Kanisa na Ulimwengu kwa ujumla baada ya takribani miaka 600! Si haba! Makardinali walioamua kumpatia dhamana ya kuliongoza Kanisa waliona ndani mwake imani thabiti ya mtu aliyekuwa na kiu ya kutafuta ukweli! Hapa akaunganisha falsafa yake kwa kusema, imani na akili ni chanda na pete na wala hakuna mgogoro.

Akili na Imani viwawezeshe waamini na watu wenye mapenzi mema, kumfahamu Yesu Kristo Mkombozi wa dunia! Joseph Ratzinger akawashangaza watu! Wakabaki wameshika kidevu! Anasema Bwana Antonio Pelayo, Balozi wa Hispania mjini Vatican. Huyu ndiye lile Jiwe ambalo lilikuwa linabezwa na waasi, lakini sasa limekuwa ni Jiwe kuu la msingi! Maajabu ya Mungu.

Joseph Ratzinger akaonesha ulimwengu kwamba, ni mtu wa kuaminika si tu kwa maneno bali zaidi katika matendo yake; wazi kwa ajili ya majadiliano ya kina, anayekubali kupokea pia ushauri kutoka kwa wengine, hata wale ambao wanaonesha upinzani wa wazi wazi! Alitambua kwamba, hata wao walikuwa na chembe ya ukweli ambayo walitaka kuishirikisha!

Bwana Antonio Pelayo anaendelea kusema kwamba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ameongoza kipindi kigumu katika historia ya Kanisa, kilichosheheni pia makwazo kama yale yaliyojionesha kuhusu unyanyasaji wa kijinsia uliofanywa na baadhi ya viongozi wa Kanisa! Ukweli na uwazi katika matumizi ya fedha za Kanisa!

Ni Kiongozi aliyesimamia kweli za Kiinjili, Maadili na Utu wema; Waswahili wanasema, mwenye macho aambiwi tazama! Katika kipindi cha miaka minane ya uongozi wake, ametoa kipaumbele cha pekee katika majadiliano ya kidini na kiekumene, akaanzisha Jukwaa la Majadiliano na wale wasioamini, lakini wana kiu ya kutaka kumfahamu Mungu.

Changamoto kubwa inayoachwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo ni Uinjilishaji Mpya unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa linalotoa ushuhuda wa maadili na utu wema, daima likionesha mshikamano wa dhati na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii!

Kanisa lijikite zaidi na zaidi katika huduma na kukoleza mchakato wa kuponya madonda ya utengano na migawanyiko ambayo kimsingi haina tija wala mafao kwa ustawi na maendeleo ya Watu wa Mungu duniani, ili watu wengi waweze kumfahamu, kumpenda na kujitoa kumtangaza Kristo, njia, ukweli na uzima!

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa anasema Bwana Antonio Pelayo, Balozi wa Hispania mjini Vatican, sasa ametoweka machoni pa ulimwengu, ili kuungana na Yesu Kristo Mkombozi wa dunia kwa njia ya sala na tafakari ya kina!







All the contents on this site are copyrighted ©.