2013-03-02 11:27:08

Wakaacha yote wakamfuata!


Yesu alipomaliza kufundisha, akamwambia Simoni, “tweka hadi kilindini, mkatupe nyavu zenu mpate kuvua samaki”. Simoni akamjibu, Bwana, tumejitahidi kuvua samaki usiku kucha bila kupata kitu, lakini kwa kuwa umesema, nitatupa nyavu. Baada ya kufanya hivyo wakavua samaki wengi, hata nyavu zao zikaanza kukatika. Wakawaita wenzao waliokuwa katika mashua nyingine waje kuwasaidia. Wakaja wakazijaza mashua zote mbili samaki, hata karibu zingezama.

Simoni Petro alipoona hayo, akapiga magoti mbele ya Yesu akisema, Ondoka mbele yangu, Ee Bwana, kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi. Simoni pamoja na wenzake walishangaa kwa kupata samaki wengi vile. Hali kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa wavuvi wenzake Simoni. Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope; tangu sasa utakuwa ukivua watu” Basi, baada ya kuzileta zile mashua ukingoni mwa Ziwa, wakaacha yote, wakamfuata.

Majina ya Mitume kumi na wawili ni haya: wa kwanza ni Simoni aitwaye Petro, na Andrea ndugu yake; Yakobo Mwana wa Zebedayo; na Yohane Ndugu yake; Filipo na Bartholomayo; Thoma na Mathayo aliyekuwa mtoza ushuru; Yakobo Mwana wa Alfayo; na Thadayo, Simon Mkaanani na Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu.

Yesu aliwatuma hao kumi na wawili na kuwapa maagizo haya: msiende kwa watu wa mataifa mengine wala msiingie katika miji ya Wasamaria, ila nendeni kwa watu wa Israeli waliopotea kama Kondoo. Mnapokwenda hubirini hivi: Ufalme wa Mbinguni umekaribia; sasa mimi ninawatuma ninyi kama Kondoo kati ya mbwa mwitu. Muwe na busara kama nyoka na wapole kama njiwa. Jihadharini na watu, maana watawapeleka ninyi mahakamani na kuwapiga viboko katika masunagogi yao.

Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, mpate kunishuhudia kwao na kwa watu wa mataifa. Basi watakapowapeleka ninyi mahakamani, msiwe na wasi wasi mtasema nini au namna gani; wakati utakapofika, mtapewa la kusema. Maana si ninyi mtakaosema, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. Kila mtu anayenikiri hadharani kwamba yeye ni wangu, mimi pia nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.








All the contents on this site are copyrighted ©.