2013-03-02 07:35:00

Kanisa linahitaji Baba, Mchungaji mkuu na Mwalimu wa Kweli za Kiinjili, Maadili na Utu wema!


Askofu mkuu Savio Hon Tai Fai, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu anasema, wakati huu Kanisa linapoendelea kusali kwa ajili ya kumwomba Roho Mtakatifu aweze kulijalia Kiongozi mkuu, atakayewaongoza watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani, wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwa sadaka na utume wake kwa ajili ya Kanisa la Kristo.

Wafanyakazi wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, wanaahidi kuendelea kumsindikiza katika sala na sadaka zao, wakati huu anapoanza hatua ya mwisho ya hija ya maisha yake hapa duniani. Alikuwa ni mtu aliyependa na kuheshimu ukweli na uwazi; akajitahidi kumwilisha Injili ya upendo katika maisha na utume wake. Alijitahidi kuponya madonda ya utengano ndani ya Kanisa, kwa kuwahamasisha waamini kujishikamanisha na Kristo kwa njia ya Sala, Tafakari na Matendo ya huruma yanayoonesha ile imani tendaji katika vipaumbele vya waamini. Aliamini na kutambua kwamba, Yesu Kristo ndiye chemchemi ya ukweli na matumaini ya binadamu.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kwa sasa anao muda mrefu zaidi kwa ajili ya kutafakari pamoja na kuliombea Kanisa. Ni wajibu wa kila mwamini kuendelea kuwa mwaminifu kwa Kristo na Kanisa lake sanjari na kuwaombea Makardinali wanaoanza mchakato wa uchaguzi wa Khalifa Mpaya wa Mtakatifu Petro, kutekeleza dhamana hii nyeti kwa ajili ya mafao ya Kanisa zima. Kanisa linamhitaji kiongozi atakayekuwa na fadhila za kibaba, mchungaji mkuu anayeonesha njia na mwalimu atakayefundisha kweli za Kiinjili, Maadili na Utu wema!







All the contents on this site are copyrighted ©.