2013-03-02 11:31:41

Atakayevumilia hadi mwisho...!


Siku ile Yesu akatoka nyumbani, akaketi kando ya bahari. Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni, akaketi; nau le mkutano wote wakasimama Pwani. Yesu alifundisha kwa mifano mingi: juu ya Mpanzi na kuwafafanulia maana ya mifano hii kadiri ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Anasema, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona, lakini wasiyaone; na kuyasikia mnayosikia lakini wasiyasikie! Yesu akafafanua kwa kina kuhusu Magugu, Punje ya haradali, Chachu na kwamba, hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano, wala pasipo mfano hakuwaambia neno, ili litimie neno lililonenwa na Nabii, akisema ”nitafumbua kinywa changu kwa mifano, nitayatamka yaliyositirika tangu awali.

Katika mifano yote hii Yesu anakazia umuhimu wa kutubu na kuongoka kwa kujivika fadhila ya unyenyekevu kama watoto wadogo. Anazungumzia kuhusu makwazo na kuwaonya wote wanaowakwaza wengine kwamba, kwa hakika watakiona cha mtema kuni! Anawaalika kuonyana kidugu, kusali pamoja na kusameheana wao kwa wao wakitambua kwamba, Bwana yu kati yao!

Yesu anawaonya wafuasi wake dhidi ya chachu ya Mafarisayo, bali ushuhuda wao ujioneshe katika maneno na matendo. Yesu pia alichukua fursa ile kukemea mji wa Yerusalem ambao pia unasifika kwa kutenda mauaji ya Manabii waliotumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Yesu anawataka wafuasi wake wasidanganyike na Manabii wa uwongo, dhuluma na taabu mbali mbali watakazokutana nazo.

Lakini atakayevumilia hadi mwisho, huyo ndiye atakayeokoka. Tena habari Njema ya Wokovu itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja! Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu anasema Yesu hayatapita kamwe! Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata Malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake.








All the contents on this site are copyrighted ©.