2013-03-01 07:58:00

Zingatieni mafao ya wengi wakati wa uchaguzi nchini Kenya!


Ni matumaini ya Jumuiya ya Kimataifa kwamba, Wananchi wa Kenya watashirikiana kwa pamoja kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi, haki na amani, ili kuweza kufanikisha mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Kenya hapo tarehe 4 Machi 2013. Ni maneno ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon alipokuwa anazungumza na Rais Mwai Kibaki wa Kenya kwa njia ya simu hapo tarehe 27 Februari 2013.

Katibu mkuu anaipongeza Serikali ya Kenya kwa hatua ambazo imechukua hadi sasa katika kuimarisha mfumo wa demokrasia nchini humo. Ni matumaini ya Jumuiya ya Kimataifa kwamba, Kenya itaendelea kuimarisha juhudi za kujenga misingi ya haki, amani na utulivu wakati huu homa ya uchaguzi mkuu inapozidi kupamba moto! Kuna haja pia ya kuheshimu maamuzi ya Tume huru ya Uchaguzi ambayo imekabidhiwa dhamana ya kuhakikisha kwamba, mchakato mzima wa uchaguzi unafanikiwa na kuonesha matashi ya wananchi wa Kenya kwa njia ya kura zao.

Ni matumaini ya Katibu mkuu kwamba, matamko yaliyotolewa na Marais watarajiwa yataheshimiwa, ili kujenga na kuimarisha amani na utulivu; ukweli na uwazi.







All the contents on this site are copyrighted ©.