Yaliyojiri wakati Baba Mtakatifu Benedikto XVI anang'atuka madarakani!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jioni tarehe 28 Februari 2013 ameondoka
rasmi kama Papa kutoka mjini Vatican, baada ya kuzungumza kwa faragha na Kardinali
Tarcisio Bertone, katibu mkuu wa Vatican ambaye kwa sasa ndiye Kardinali Carmelengo,
yaani "Mlinzi".
Papa alipata fursa ya kuagana na wafanyakazi wa Vatican waliofika
kwa wingi wakiandamana pia na familia zao. Vikosi vya Ulinzi kutoka Uswiss vilitoa
heshima zao za mwisho na baadaye Baba Mtakatifu alipanda gari kuelekea Uwanja wa Ndege
wa Vatican tayari kuondoka kwenda Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo ambako kwa sasa anapumzika
baada ya kulitumikia Kanisa kwa miaka minane kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Hili
ni tukio ambalo limevuta hisia za watu wengi waliokuwa wamekusanyika kwanza kabisa
kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kushuhudia tukio hili la kihistoria
lililokuwa linarushwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha Vatican hadi alipowasili
kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo. Alipopita juu ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro,
Makao makuu ya Jiji la Roma, Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano pamoja na
Makanisa kadhaa, kengele ziligonjwa kama kielelezo cha kumsindikiza Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita.
Waamini na watu wenye mapenzi mema waliendelea kufuatilia
tukio hili hadi pale ilipofika majira ya saa 2:00 Usiku, lango kuu la Ikulu Ndogo
ya Castel Gandolfo lilipofungwa na Askari wa Kiswiss wakakabidhi dhamana ya ulinzi
na usalama kwa Vikosi vya Usalama vya Vatican. Maaskari wa Kiswiss wamerudi Vatican
ili kuendelea kutoa huduma yao kwa Makardinali ambao kwa sasa wako kwenye pilika pilika
za kuanza mchakato wa kumchagua Papa Mpya. Ni tukio ambalo limewaacha watu wengi wakiwa
wameshikwa na butwaa kwa kutoamini maamuzi magumu yaliyofanywa na Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita!