2013-03-01 07:25:25

Siku ya Watu wa Amerika ya Kusini: lengo kukuza na kuimarisha umoja, mshikamano katika Uinjilishaji Mpya!


Kunako mwako 1959 Kanisa lilianzisha Siku ya Watu wa Amerika ya Kusini, inayoadhimishwa kila Mwaka ifikapo tarehe 3 Machi. Lengo ni kukuza na kuendeleza mchakato wa umoja, mshikamano na ushirikiano katika Uinjilishaji, kati ya Hispania na Nchi za Amerika ya Kusini. RealAudioMP3

Katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, sanjari na Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, waamini wanaoishi Amerika ya Kusini wanakumbushwa kwamba, hili ni eneo ambalo malango yake yako wazi kwa ajili ya Uinjilishaji.

Ni mwaliko kwa kila mwamini kukumbuka ile dhamana ya kutangaza Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake pamoja na kushiriki katika kuendeleza harakati za kimissionari sehemu mbali mbali za dunia, kwani wakumbuke daima kwamba, ni upendo wa Kristo unaowasukuma Kuinjilisha. Haya ni maneno ya Kardinali Marc Ouellet, Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini katika ujumbe wake kwa Maadhimisho haya. Juhudi za kimissionari ni kigezo muhimu sana kinachoonesha uhai wa Kanisa na Jumuiya zake za Kikristo.

Takwimu zinaonesha kwamba, walau asilimia 50% ya Waamini wa Kanisa Katoliki wanaishi Amerika ya Kuini. Hii ndiyo imani ambayo imepelekea Kanisa Katoliki kuwa na idadi kubwa ya Mapadre na Watawa kutoka Amerika ya Kusini, utume na dhamana iliyofanywa na wadau mbali mbali wa Injili kutoka Hispania. Juhudi za Uinjilishaji mpya anasema Kardinali Ouellet zinajikita hasa zaidi katika toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Kuna mabadiliko makubwa yanayogusa medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu; Njia za mawasiliano ya Kijamii zimekuwa ni majukwaa mengine yanayopaswa Kuinjilishwa ili yaweze kukumbatia kweli za Kiinjili na tunu bora za maisha na utu wa mwanadamu.

Maendeleo haya pia yameibua kundi kubwa la maskini na watu wasiokuwa na ajira, hali ambayo inaendelea kusababisha shida na mahangaiko makubwa ya watu sehemu mbali mbali za dunia, hususan kwenye miji mikubwa. Kuna wazee waliokata tamaa, wasiokuwa na matumaini tena kutokana na kupanda kwa gharama za maisha na kushuka kwa hali ya maisha; ni watu wanaokosa huduma msingi za tiba na malazi; hao ndio wanaoteseka na baridi pamoja na joto katika mitaa ya miji mikubwa duniani. Kumekuwepo na ongezeko la nyanyaso kwa wanawake na wasichana, hali inayowatumbukiza hata katika utumwa mamboleo.

Kutokana na kukabiliana na hali ngumu ya maisha, vijana wengi wamejikuta wakijitumbukiza katika matumizi haramu ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia pamoja makosa ya jinai. Kundi la vijana wasiokuwa na fursa za ajira ni hatari kwa maisha, ustawi na maendeleo ya Jamii, kwani wanaweza kutumiwa na watu wasiokuwa na nia njema kuleta machafuko kama inavyojionesha sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Marc Ouellet anasema licha ya kundi kubwa la wananchi kutopea katika umaskini wa kipato na kihali, lakini kuna baadhi ya watu wanaoendelea kuponda maisha, huku “wakila kuku kwa mirija”! Ni watu wanaojibovusha kwa starehe na anasa pamoja na kuendelea kuzama katika wimbi la mmong’onyoko wa kimaadili na utu wema. Mazingira kama haya yanaendelea kuhatarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kiasi kwamba, watu wanaanza kujikuta wakikimbatia utamaduni wa kifo, unaowaacha watoto na vijana wakiwa yatima; wakikosa malezi bora na makini kutoka kwa wazazi na walezi wao! Hawana mifano bora ya kuigwambele yao!

Utepetevu wa imani, maadili na utu wema ni mwaliko na changamoto ya pekee katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kutubu na kuongoka, ili waamini waweze kuwa kweli ni wafuasi amini wa Kkristo kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa matendo yao yanayoonesha ile imani tendaji na kwa njia hii, watu wengi wataweza kumfahamu tena Kristo.

Toba na wongofu wa ndani uguse mihimiri ya shughuli na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na kuamsha tena ari na moyo wa kimissionari ili kuweza kuwashirikisha wengine ile furaha ya kukutana na Yesu katika Maandiko Matakatifu, Maisha ya Kisakramenti na Matendo ya Huruma. Waamini wajenge moyo wa upendo na mshikamano na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii na kwa namna ya pekee wahamiaji na wageni.

Vyama vya kitume viendelee kutekeleza wajibu na majukumu yao ya kila siku kwa, kwa kuwashirikisha waamini walei ambao wanadhamana nyeti ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda amini wa maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake. Watawa na Makleri washirikiane kwa karibu zaidi na waamini walei katika utekelezaji wa dhamana na utume wa Kanisa katika Uinjilishaji Mpya.

Kardinali Marc Ouellet, Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini anahitimisha ujumbe wake kwa kuwataka waamini wote kushirikiana kwa na kujitoa bila ya kujibakiza katika maisha na utume wa Kanisa.








All the contents on this site are copyrighted ©.