Rais Kikwete azungumzia uhusiano kati ya Waislam na Wakristo Tanzania
Ndugu wananchi; Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujalia uzima
na kutuwezesha kuwasiliana kupitia utaratibu wetu mzuri tuliojiwekea wa kufanya hivyo
kila mwisho wa mwezi. Leo nimepanga kuzungumza nanyi mambo matatu; yaani Mpango wa
Amani, Usalama na Ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Uhusiano wa Waislamu
na Wakristo na Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne.
Mpango wa Amani,
Usalama na Ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
Ndugu
Wananchi; Tarehe 8 Februari, 2013 kule Addis Ababa, Ethiopia niliungana na Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Ban Ki-Moon, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika,
Mhe. Nkosozana Dlamini Zuma na viongozi wa nchi 12 za Afrika Mashariki, Kati na Kusini
kutia saini Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
na jirani zake. Pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zilikuwepo nchi za Burundi,
Rwanda, Uganda, Sudani Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Angola,
Zambia na Tanzania ambazo ni jirani ya Kongo. Nchi za Ethiopia, Msumbiji na Afrika
ya Kusini pamoja na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zilitia saini kama wadhamini.
Ethiopia kwa nafasi yake ya kuwa Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika na Msumbiji
kwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Nchi wanachama
wa Mkutano wa Ukanda wa Maziwa Makuu ziliwakilishwa na Uganda ambayo ni Mwenyekiti
wake wa sasa. Afrika ya Kusini ilishirikishwa kwa kuwa taifa kubwa na linalotegemewa
katika ukanda wetu.
Mpango huu ni jitihada nyingine ya kusaidia Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo ipate amani ya kudumu. Kama tujuavyo, tangu mwaka 1997 wakati
wa vita vilivyosababisha kuondolewa kwa Rais Mobutu Seseseko mpaka sasa nchi hiyo
rafiki na jirani haijapata amani na utulivu wa kudumu. Kumekuwepo jitihada na mipango
kadhaa ya kuleta amani ambayo hata hivyo baada ya muda fulani machafuko hutokea tena
na mipango hiyo kuvurugika. Inakadiriwa kuwa takriban watu milioni 5.4 wamepoteza
maisha na watu wengi kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi yao. Pia kumekuwepo na vitendo
vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na mali nyingi kuharibiwa au kuporwa.
Ndugu
Wananchi; Machafuko yaliyoanzishwa na waasi wa Kundi la M23 mapema mwaka wa jana
ndiyo sababu ya kuwepo kwa Mpango huu wa sasa tuliotia saini kule Addis Ababa, Ethiopia
tarehe 8 Februari, 2013. Katika Mpango huo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na jirani
zake, Tanzania ikiwemo, tumekubaliana kutokufanyiana vitendo vinavyohatarisha amani
na usalama wa nchi zetu. Tumeazimia tusifanye hivyo ama moja kwa moja kama nchi au
kwa kutumia watu wengine. Aidha, tumekubaliana tusiruhusu watu au vikundi vya watu
kutumia nchi zetu kuhatarisha usalama wa nchi nyingine. Kimsingi tumekubaliana kuwa
majirani wema. Katika Mkataba huo, majukumu ya kila nchi yameainishwa vizuri pamoja
na yale ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Mashirika ya Kikanda hususan SADC
na ICGLR.
Ndugu Wananchi; Niliamua kukubali kushiriki na kutia saini Mpango
ule kwa kutambua ukweli kwamba sisi majirani wa nchi ya Kongo tunao wajibu wa kusaidia
kwa kile tunachoweza. Wananchi wa Kongo wameteseka kwa muda mrefu mno hivyo kama
Mpango huu utawasaidia kupata amani na usalama hatuna budi kuunga mkono. Ni kwa misingi
hiyo hiyo, tulikubali kuchangia kikosi kimoja katika Jeshi la Kimataifa la kulinda
amani huko Mashariki ya Kongo kama ilivyoamuliwa na Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu
mwezi Julai, 2012. Uamuzi huo umeungwa mkono na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika
na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika. Umoja wa Mataifa umeamua Jeshi hilo
liwe sehemu ya Jeshi la Umoja wa Mataifa la Kulinda Amani nchini Kongo (MONUSCO) jambo
ambalo sote tumeliafiki. Tumepeleka walinzi wa amani Darfur, Sudan na Lebanon, kwa
nini tusipeleke Kingo. Miaka ya nyuma tulishapeleka walinzi wa amani Liberia, Siera
Leon na Eritrea.
Ni matumaini yetu kuwa Mpango huu mpya utatekelezwa kwa ukamilifu
na kuzaa matunda yaliyokusudiwa. Kama nchi jirani, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
yenye amani, usalama na utulivu ni jambo lenye maslahi makubwa kwetu. Ina maana ya
kutokuwa na wakimbizi kutoka nchi hiyo, uharamia katika Ziwa Tanganyika kutokuwepo
na ustawi wa shughuli za kiuchumi na kibiashara kwa upande wetu na wao. Ni chachu
muhimu ya maendeleo ya Mikoa ya pembeni mwa Ziwa Tanganyika na Tanzania kwa jumla.
Uhusiano
wa Waislamu na Wakristo
Ndugu wananchi; Jambo la pili
ninalopanga kulizungumzia siku ya leo ni uhusiano wa Wakristo na Waislamu hapa nchini.
Kwa miezi kadhaa sasa tangu mwaka wa jana kumekuwepo na matukio kadhaa yanayosababisha
mifarakano na kupandikiza chuki baina ya waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu.
Matukio ya kauli na vitendo vya kudharau dini za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu
vya dini hizo, kuchoma moto nyumba za ibada na mzozo kuhusu nani achinje. Kumekuwepo
na matumizi mabaya ya radio na simu za mkononi na mifumo mingine ya mawasiliano iliyoeneza
maneno na ujumbe wa chuki na vitisho kwa waumini na viongozi wa dini zetu hizi kubwa
hapa nchini. Kauli na matendo hayo, katika baadhi ya maeneo yamekuwa chanzo cha uhasama
na magomvi baina ya waumini na hatimaye kusababisha vifo kama ilivyotokea Buseresere
Mkoani Geita na Beit-el-Ras, Zanzibar.
Ndugu zangu;
Watanzania hatujawahi kuwa hivi, kumetokea nini? Miaka yote Watanzania ni watu tunaotambua
na kuheshimu tofauti za dini zetu mbalimbali tunazoabudu. Watanzania ni waelewa na
kwa ajili hiyo tumekuwa tunavumiliana kwa tofauti zetu na ndiyo maana tumekuwa tunaishi
pamoja kidugu, kwa umoja na kushirikiana kwa mambo yote yanayotuhusu maishani isipokuwa
wakati kila mmoja anapoingia kwenye nyumba ya ibada kumuomba Mola kwa misingi na taratibu
ya dini yake.
Watanzania wa dini zote na makabila tofauti wanaishi nyumba
moja, wanasoma pamoja, wanafanya kazi pamoja kwa udugu, upendo, umoja na ushirikiano.
Kuna koo na familia zenye watu wa dini tofauti, wengine Waislamu na wengine Wakristo.
Wapo Waislamu na Wakristo wameoana, wamezaa na wamejukuu na kila mmoja amebakia kuwa
mfuasi wa dini yake. Wapo pia ambao hawakuoa lakini wamezaa watoto na wanashirikiana
kulea watoto wao. Hayo ndiyo maisha ya Watanzania na hiyo ndiyo Tanzania yenye amani
na utulivu tuliyozaliwa, kukua na kuishi. Nawasihi sana Watanzania wenzangu, tuienzi
na kuidumisha tunu hii waliyotujengea mababu zetu.
Ndugu Wananchi;
Kuna wenzetu kwa sababu wanazozijua wao na kwa manufaa wanayoyajua wao wanataka kutuvurugia
nchi yetu hii nzuri. Tusiwape nafasi wachochezi hawa kwani hawatutakii mema na wala
hawazitakii mema dini zetu na nchi yetu. Sisi katika Serikali hatutasita kuwachukulia
hatua wale wote wanaochochea chuki za kidini, wanaodharau vitabu vitakatifu vya dini
nyingine na wanaokejeli dini nyingine.
Nimewakumbusha Polisi na mamlaka husika
kote nchini wasifanye ajizi kwenye matukio ya namna hiyo. Wawachukulie hatua stahiki
wale wote wanaohusika. Nimewataka wazingatie msemo wa Kiswahili usemao “ajizi nyumba
ya njaa”. Wachochezi wa mifarakano na chuki za kidini wasipodhibitiwa ipasavyo wataleta
maafa kwa Watanzania wasiokuwa na hatia. Nimewakumbusha Wakuu wa Wilaya na Mikoa
kama walinzi wa amani wa maeneo yao ya uongozi, watimize ipasavyo wajibu wao. Pia
nimewataka Polisi wakamilishe mapema upelelezi wa makosa ya vurugu za kidini na wahusika
wafikishwe haraka kwenye vyombo vya sheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Ndugu
Wananchi; Naendelea kuwasiliana na viongozi wa dini kuzungumza nao juu
ya wajibu wao maalum wa kuhakikisha kuwa wafuasi wao hawawi chanzo au sehemu ya tatizo
na mifarakano miongoni mwa waumini wa dini mbalimbali nchini. Hali kadhalika naitumia
nafasi hiyo kuwakumbusha umuhimu wa kuzungumza na wenzao wa upande mwingine kutatua
tofauti au matatizo yanayoathiri uhusiano mwema baina yao.
Ndugu Wananchi;
Kuna msemo maarufu usemao “mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi”.
Naomba tuwe wajenga nchi na kamwe tusikubali kuwa wabomoa nchi. Hivi tukiibomoa nchi
yetu tutakwenda wapi? Tutaishi wapi? Tusikubali kugeuka wakimbizi ndani ya nchi au
nje ya nchi yetu.
Kwa mara nyingine tena, napenda kutumia nafasi hii kuwapa
mkono wa pole makanisa, familia, ndugu na jamaa wote wa Mchungaji Kachila na Padri
Mushi. Sote tunafahamu machungu waliyonayo kwa kuondokewa na wapendwa wao. Serikali
na wapenda amani wote nchini wapo pamoja nanyi katika kipindi hiki kugumu. Vile vile
natoa rambirambi zangu nyingi kwa waumini wote wa Kanisa la Pentekoste Assemblies
of God na Kanisa Katoliki Tanzania kwa kuondolewa ghafla na viongozi wao. Tuzidi kumwomba
Mwenyezi Mungu azipumzishe kwa amani roho za viongozi wetu. Amin.
Matokeo
ya Mtihani wa Kidato cha Nne Mwaka 2012
Ndugu wananchi; Tarehe
18 Februari, 2013 Baraza la Mitihani la Taifa lilitangaza matokeo ya Mtihani wa Taifa
wa Kidato cha Nne ya mwaka 2012. Wanafunzi 397,132 walifanya mtihani huo na kati
ya hao, waliofaulu ni 126,851 yaani sawa na asilimia 34.5. Wanafunzi 240,903 ambao
ni sawa na asilimia 65.5 hawakufaulu mtihani huo. Kwa ulinganifu, matokeo hayo ni
mabaya kuliko matokeo mengine ya mtihani huo ya miaka ya hivi karibuni.
Mwaka
2011, jumla ya wanafunzi 336,782 walifanya mtihani huo na waliofaulu walikuwa asilimia
53.6 na ambao hawakufaulu kabisa walikuwa asilimia 46.4. Mwaka 2010 jumla ya wanafunzi
352,045 walifanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne, asilimia 50.4 ya wanafunzi hao
walifaulu na asilimia 49.6 ya wanafunzi hawakufaulu.
Ndugu Wananchi;
Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012, yameshtua na kufadhaisha watu wengi
nchini na kwa sababu stahiki kabisa. Kwanza, kwamba kiwango cha kufaulu kimeporomoka
sana, tena ghafla, kutoka asilimia 53.6 mwaka 2011 hadi asilimia 34.5 mwaka 2012.
Hili ni anguko la asilimia 19.1 ambalo, kwa kila hali, ni kubwa sana. Pili, kwamba
hata shule zinazofahamika kuwa na historia ya kufaulisha vizuri kama vile seminari,
shule za watu binafsi, za mashirika ya dini na sekondari kongwe za Serikali ambazo
hazina matatizo kama ilivyo kwa zile sekondari za Kata, nazo safari hii hazikupata
mafanikio kama ilivyo kawaida yao. Nazo zimejikuta zikiwa na idadi ya vijana waliopata
daraja la kwanza, la pili na la tatu ikipungua wakati waliopata daraja la nne na
waliofeli wakiongezeka.
Isitoshe na kiwango cha ufaulu wa vijana umepungua
pia. Mwaka 2010 wanafunzi 10 bora wote walikuwa wamefaulu daraja la kwanza la alama
au pointi 7. Mwaka 2011 katika wanafunzi 10 bora wanane walipata daraja la kwanza
kwa alama 7 na wawili alama 8. Mwaka 2012 katika wanafunzi 10 bora, watatu walipata
daraja la kwanza kwa alama 9, watatu alama 10 na wawili alama 11.
Ndugu
Wananchi; Haya ndiyo mambo yanayozua maswali kwa watu wengi yanayohitaji kupatiwa
majawabu ya uhakika. Kulikoni mwaka 2012? Ndiyo msingi wa uamuzi wa Waziri Mkuu,
Mhe. Mizengo Pinda, kuamua kuunda Tume ya kuliangalia suala zima la mitihani ya mwaka
2012 na matokeo yake. Hali hii haijawahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni.
Ni suala muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu, hivyo lazima ukweli wake ujulikane
kwa uhakika. Hii itawezesha Serikali na wadau wengine kuchukua hatua stahiki kurekebisha
mambo mapema iwezekanavyo ili hatimaye mambo yawe mazuri siku za usoni. Tusipofanya
hivyo mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi na lawama zinaweza kuwa kubwa zaidi kwa Serikali.
Ndugu
Wananchi; Hivi sasa kunatolewa mawazo lukuki kuhusu sababu za kwa nini
matokeo yamekuwa mabaya. Wapo wanaodhani kuwa lipo tatizo katika utungaji wa mitihani,
usahihishaji wake au kutoa maksi kwa watahiniwa. Wapo wanaodhani walimu hawawajibiki
ipasavyo au baadhi yao kutokumudu masomo wanayofundisha. Wapo wanaofikiria kuwa wanafunzi
hawako makini katika kufuatilia masomo na wazazi hawajali kufuatilia maendeleo ya
watoto wao shuleni. Wapo wanaoinyooshea kidole Serikali kwa sera, mitaala na uwekezaji
usiokidhi mahitaji ya maendeleo ya elimu. Wapo wanaofikiria kuwa Serikali kushindwa
kuongeza mishahara ya walimu kwa asilimia 100 kama walivyotaka imechangia.
Orodha
ni ndefu, ali mradi kila mtu ana mawazo yake. Na sisi katika Serikali hatuwezi kuwa
tunadhani kwa sababu tunayo dhamana maalum. Lazima tujue ukweli kwa uhakika na ndiyo
maana kuna umuhimu wa Tume. Naomba kila mtu mwenye mawazo yake ayafikishe kwenye
Tume hiyo hapo itakapoundwa ili tupate jawabu muafaka la tatizo hili.
Ndugu
Wananchi; Napenda kuwahakikishia kuwa sisi katika Serikali tumetoa kipaumbele
cha juu sana kwa elimu na kwamba hakuna upungufu wa utashi kwa upande wangu na wenzangu
wote Serikalini. Ndiyo maana tumeguswa sana na matokeo haya. Bajeti ya elimu ya
shilingi trilioni 3.6 ambayo ni sawa na asilimia 24 ya bajeti yote ya Serikali ndiyo
kubwa kuliko zote. Kwa ajili hiyo imetuwezesha kuendelea kukabili mahitaji na changamoto
za upanuzi mkubwa wa elimu ya sekondari na elimu ya juu. Bado hatujazimaliza changamoto
zote na kwamba bado tuna kazi kubwa mbele yetu, lakini mafanikio yanaendelea kupatikana.
Tutaendelea kutoa kipaumbele cha juu kwa elimu mpaka hapo itakapofikia mahali kwamba
matatizo makubwa yatakapokuwa yamepungua sana.
Hitimisho
Ndugu
Wananchi;
Mungu Ibariki Tanzania! Mungu Ibariki Afrika! Nashukuru
kwa kunisikiliza!