Baada ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuamua kung'atuka kutoka madarakani,
baada ya kuliongoza Kanisa kwa kipindi cha miaka minane, sasa kiti cha Ukulu wa Mtakatifu
Petro kiko wazi. Kama Familia ya Wasalesiani wa Mtakatifu Bosco, wanatambua na kuthamini
mchango wa Papa Benedikto wa kumi na sita, mwaliko wa kuendelea kusali kwa ajili yake.
Ni
maneno ya Mheshimiwa Padre Pascual Chavez, Mkuu wa Shirika la Wasalesiani, anayemshukuru
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, ambaye amekuwa kweli ni zawadi kubwa
ya Mungu kwa Kanisa na Ulimwengu kwa ujumla. Ameonja ukarimu na uwepo wa Familia ya
Mungu, hata pale ambapo watu walidhani kwamba, "Mungu anasinzia". Wasalesiani wanapenda
kumhakikishia Baba Mtakatifu mstaafu uwepo wao wa karibu kwani Mafundisho yake yataendelea
kuhifadhiwa katika sakafu za mioyo yao!
Kwa wakati wake, historia itatoa hukumu
ya maisha na utume wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwa kuonesha
ukuu wa binadamu, akili na maisha thabiti ya kiroho. Upendo wake kwa Kristo na Kanisa
lake, utaendelea kung'ara miongoni mwa Familia ya Mungu na kwamba, amejitoa bila ya
kujibakiza kwa ajili ya kulihudumia Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Yeye mwenyewe
anawakumbusha waamini kwamba, Kanisa haliwezi kubaki kama mtoto yatima kwani, Kristo
ni kichwa cha Kanisa linaloongozwa kwa nguvu za Roho Mtakatifu.
Wasalesiani
wanaalikwa kuungana na Kanisa zima kwa ajili ya kusali ili kuombea mchakato wa uchaguzi
wa Papa Mpya, kadiri ya mpango wake. Katika kipindi cha Kwaresima, toba na wongofu
wa ndani ni mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee, ndivyo Mheshimiwa Padre Pascual
Chàvez, Mkuu wa Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco anavyohitimisha ujumbe wake kwa
ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita pamoja na kuombea
mchakato wa uchaguzi wa Papa mpya!