Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Alhamisi tarehe 28 Februari 2013 ametuma
salam za rambi rambi kwa Askofu mkuu Bernard- Nicolas Aubertin wa Jimbo kuu la Tours,
Ufaransa kufuatia kifo cha Kardinali Jean Marcel Honore, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo
kuu la Tours, aliyefariki dunia hapo tarehe 28 Februari 2013 akiwa na umri wa miaka
92.
Baba Mtakatifu katika salam zake za rambi rambi anasema kwamba, Kardinali
Honore alikuwa ni kiongozi aliyelihudumia Kanisa kwa kujitoa bila ya kujibakiza, hasa
katika sekta ya elimu na katekesi ya kina. Anaiombea roho ya Marehemu kardinali Honore
iweze kupokelewa amani na mwanga wa milele. Itakumbukwa kwamba ni kati ya viongozi
waliohariri Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki, kwa ari na moyo mkuu akitamani daima
kutangaza Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia!