Ibada ya Kukabidhiana Msalaba wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Jimbo kuu la
Dar es Salaam
Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Msalaba unachukua maana ya pekee katika maisha
ya waamini, kwani wanatumwa na kuchangamotishwa kuwa ni mashahidi amini wa Kristo
na Kanisa lake: kwa maneno na matendo. Msalaba ni kielelezo cha mapendo, neema, sala,
msamaha na matumaini yasiyodanganya kamwe!
Ndiyo maana, Kanisa linaona fahari
juu ya Msalaba wa Kristo kwa kuutembeza katika nyumba za waamini, ili wapate nafasi
ya kusali na kulitafakari Fumbo la Msalaba, ishala ya mateso na alama ya wokovu wa
binadamu; mahali ambapo hekima ya Mungu imetundikwa juu yake! Ni mwaliko wa kutubu
na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Ifuatayo ni Ibada ya kukabidhiana Msalaba katika Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Vikundi vya pande zote mbili:
wanaokabdhi na waokabidhiwa wanasimama mbele ya Msalaba. Padri wa kikundi kinachokabidhi
msalaba anaanza ibada:
Padri: Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu... Wote: Amina. Padri:
Bwana awe nanyi.. Wote: Na awe rohoni mwako.
Padri anaeleza madhumuni ya
kukutana:
Padri: Ndugu zangu, tumekutana hapa ili kukabidhiana Msalaba wa
Mwaka wa Imani, ambacho ni chombo alichotumia Bwana wetu Yesu Kristo kutukomboa. Tunafanya
tendo hili la ibada ya kuuheshimu Msalaba ili Mungu azidi kutujalia neema ambazo Kristo
alitustahilisha kwa mateso, kifo na ufufuko wake. Tunawakabidhi Msalaba huu ili muupokee
kama kumpokea Kristo mwenyewe katika parokia yenu. Uwe ishara ya ujio wake Kristo
katika Mwaka huu wa Imani. Wakati wote utakaokuwa parokiani kwenu utunzwe na kuheshimiwa
kama chombo kitakatifu kilicholeta wokovu. Ishara ya Msalaba huu iwaletee wingi wa
neema za Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu. Wote: Amina.
Sasa tusikilize
somo linalotueleza kuwa Yesu Kristo ni Mwokozi wa ulimwengu:
Somo: Yohane (3:14-21)
Inafuatia
tafakari fupi
Sala za Waamini:
Padri wa kikundi kinachopokea Msalaba
anaongoza Sala za Waamini:
Padri: Ndugu zangu, Yesu Kristo amemtolea Mungu
Baba maisha yake Msalabani ili ampatanishe na wanadamu. Ee Baba wa huruma uyasikie
maombi yetu... Wote: Bwana utuongezee imani Msalaba utukumbushe
mapendo makubwa ya Kristo; Msalaba uamshe shukrani mioyoni mwetu... Msalaba uwe
bendera ya Wakristo na alama ya ushindi wao; Msalaba ututie nguvu katika mateso, vitisho
na hatari... Msalaba utufanye tuwe imara katika imani yetu, uwe nguvu yetu ya kuwafukuza
pepo wabaya na washawishi... Msalaba uwe nguvu yetu ya kututoa katika dhambi na
mazingira ya dhambi, ili sisi sote tuweza kuingia katika ufalme wa Mungu... Kwa
ishara ya Msalaba tuwabariki wana familia zetu; tufanye ishara ya Msalaba maishani
na kifoni...
Ee Mungu, umeweka Msalaba uwe ishara ya ukombozi wetu na
alama ya huruma na mapendo yako. Twakuomba utupe neema ya kuuchukua Msalaba wetu pamoja
na Mkombozi kwa mapendo makubwa. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Wote: Amina.
Wanakabidhiana
Msalaba Mtakatifu, huku ukiimbwa wimbo ufaao...