Hili ni tukio la: kushangaza, kihistoria na kibinadamu! Atakumbukwa na wengi!
Rais Giorgio Napolitano wa Italia, kwa mara nyingine tena kwa niaba ya wananchi wa
Italia, amemshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa upendo na mshikamano
aliowaonesha wananchi wa Italia wakati wa uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Ni kiongozi ambaye amechangia mafao ya wengi si tu ndani ya Kanisa bali katika medani
mbali mbali za maisha ya kijamii. Wengi wameonja na kuguswa na ule ukawaida wa maisha
yake na kwamba, ni mtu ambaye hakupenda makuu!
Rais Nalipotano anasema, miaka
minane ya uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Vatican na Serikali ya Italia
vimeweza kushirikiana kwa karibu zaidi, katika misingi ya amani na utulivu; daima
kila upande ukipania kushirikiana kwa dhati kwa ajili ya mafao ya pande hizi mbili.
Kwa hakika amechangia kwa namna ya pekee katika ustawi wa maisha ya kiroho kwa waamini
wengi, dhamana ambayo ameitekeleza kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Rais Napolitano
anasema alikuwa na uhusiano wa kirafiki na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.
Ameonja ujasiri na moyo mkuu pale Papa alipokuwa anakabiliana na magumu katika maisha
na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro; lakini akaonesha pia imani, matumaini
na upendo mkuu kwa Kristo na Kanisa lake, kwa maneno machache Papa Benedikto wa kumi
na sita, alikuwa ni mtu wa imani thabiti. Kama viongozi, kwa pamoja waliweza kuchambua
hali za maisha ya watu wao Ulaya na Duniani kwa ujumla; wakaheshimiana na kuthaminiana,
hasa katika kukuza na kudumisha umoja wa kitaifa.
Rais Giorgio Napolitano anasema
kwamba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kung'atuka kutoka madarakani ni tukio
la kushangaza, kihistoria na kibinadamu. Anasema, bado wataendelea kumsindikiza kwa
njia ya sala katika hija ya maisha yake hapa duniani.