Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Alhamisi, tarehe 28 Februari 2013 amekutana
na kusalimiana na Makardinali 144 ambao tayari wako mjini Vatican kushiriki katika
mchakato wa kumchagua Papa mpya baada ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita,
kung'atuka rasmi kutoka madarakani, tarehe 28 Februari 2013, saa 2:00 Usiku, tukio
ambalo litarushwa moja kwa moja kutoka Castel Gandolfo.
Baba Mtakatifu pia
amepata fursa ya kukutana na kusalimiana na viongozi waandamizi kutoka Mabaraza ya
Kipapa, Washereheshaji na baadhi ya Wafanyakazi kutoka Sekretarieti ya Vatican ambao
kwa takribani miaka minane wamefanya naye kazi bega kwa bega. Baba Mtakatifu katika
hotuba yake ya mwisho kwa Makardinali amefafanua maana ya Kanisa, dhana ambayo Baba
Mtakatifu mwenyewe alijitahidi kuiishi katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu
Petro.
Baba Mtakatifu amewakumbusha Makardinali kwamba, kati yao kulikuwemo
Papa Mpya, ambaye tangu wakati huu anaahidi kumpatia heshima na utii mkamilifu. Huu
ni mwelekeo ambao Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita amependa kuuonesha kwa
Makardinali hata kabla ya kukamilika mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya, uchaguzi ambao
kimsingi hatahusika hata kidogo.
Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali
amewaambia Makardinali kwamba, tarehe Mosi, Machi, atawatumia rasmi barua za mwaliko
wa kushiriki kwenye mkutano wa Dekania ya Makardinali wenye dhamana ya kumchagua Papa
Mpya. Makardinali watashiriki katika mkutano huu kwa kufuata umri na mwaka walioteuliwa
kuwa Makardinali na baadaye watafuata Madaraja yao; yaani: Makardinali Maaskofu ambao
wamepangia utume katika Makanisa makuu yaliyoko Jimbo kuu la Roma.
Kuna Makardinali
Mapadre, hawa ni wale waliopangiwa utume kwenye Parokia za Jimbo kuu la Roma, hawa
ni Maaskofu wakuu wa Majimbo makuu kutoka sehemu mbali za dunia. Mwishoni, kuna Makardinali
Mashemasi wanaotekeleza utume wao ndani ya Vatican kama wakuu wa Mabaraza ya Kipapa.
Ufafanuzi
huu umetolewa na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican. Anabainisha kwamba,
kuna jumla ya waandishi wa habari 3,641, wanaozungumza lugha 24 kutoka katika mataifa
61. Baadhi ya waandishi wa habari ni wale ambao wamesajiliwa kwa muda.