Wanawake Wakatoliki wanamshukuru Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa kusimama kidete
kulinda na kutetea wito wa wanawake katika Kanisa na Jamii
Wanawake wana mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa kama ilivyo hata katika
Jamii. Wanawake wanapaswa kuwa waaminifu kwa mpango wa Mungu, utu na heshima yao,
daima wakijikita katika haki na usawa na kukataa katu katu aina zote za nyanyaso dhidi
ya wanawake.
Ni maneno ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika
nyaraka zake za kichungaji ambayo yanatumiwa wakati huu na Shirikisho la Vyama vya
Wanawake Wakatoliki kumshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa kuwatia
shime kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.
Wanawake Wakatoliki
wanaahidi kuendelea kumwombea Baba Mtakatifu anapoanza maisha mapya baada ya kuliongoza
Kanisa kwa miaka minane. Wanamshukuru kwa kuwachangamotisha kutangaza Injili ya Kristo
sanjari na kugundua hazina ya imani kwa kuitolea ushuhuda amini.
Wanawake kwa
unyenyekevu mkuu wanamwomba Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuwakumbuka
katika sala zake, wanapoendelea kujibidisha katika utekelezaji wa mchakato wa Uinjilishaji
mpya sehemu mbali mbali za dunia kwa kushirikisha wito na karama walizokirimiwa na
Mwenyezi Mungu. Wanamwombea amani na utulivu wakati huu anapoanza ukurasa mpya wa
maisha yake!