2013-02-28 08:05:30

Jamii inachangamotishwa kujikita katika ujenzi wa haki, amani na upatanisho!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika mafundisho yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ameendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika kulinda na kudumisha; utu, heshima, maisha na haki msingi za binadamu. RealAudioMP3

Baba Mtakatifu amekuwa ni sauti ya wanyonge, inayowaalika watu kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha ya mwanadamu tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Hatua za maisha ya mwanadamu zinapaswa kuheshimiwa, kulindwa na kuendelezwa dhidi ya utamaduni wa kifo.

Katika mantiki hii, anaendelea kukazia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, mahali ambapo bwana na bibi wanapendana kwa dhati na matunda ya upendo huu ni watoto ambao wana haki ya kulelewa na wazazi wa pande zote mbili kadiri ya mpango wa Mungu.

Baba Mtakatifu pia amekuwa akihimiza uhuru wa kidini kwa waamini wa dini mbali mbali duniani kwani haki hii ni mhimili wa haki nyingine zote anazopaswa kutendewa binadamu. Anakumbusha kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu, kwani hakuna haki pasi na wajibu. Itakumbukwa kwamba, kazi ni kielelezo cha utimilifu wa maisha ya mwanadamu

Haya ni kati ya mawazo mazito yaliyoibuliwa wakati wa Semina ya Siku moja iliyoandaliwa na Chama cha Vijana Wakatoliki Italia, hivi karibuni ili kupembua kwa kina na mapana ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2013; inayoadhimishwa kila Mwaka ifikapo tarehe Mosi, Januari.

Ni changamoto kwa kila mtu kuhakikisha kwamba, katika mazingira yake anaendeleza utamaduni wa amani, ili hatimaye, kujenga na kuimarisha dunia yenye haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati. Ili kuweza kupata mafanikio haya, kuna haja kwa Jamii kuwekeza zaidi katika elimu kwa kukabiliana na changamoto zote zile zinazoibuliwa katika mikakati ya kichungaji na kijamii.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Giovanni Angelo Becciu, Katibu mwambata wa masjala, Sektretarieti ya Vatican amezungumzia kuhusu kheri za Kiinjili, kwa kusema kwamba, Baba Mtakatifu anawataja wajenzi wa amani kuwa ni wale wote wanaopenda, wanaolinda na kuendeleza zawadi ya maisha na utimilifu wa binadamu. Jumuiya ya Kimataifa inaweza kujenga na kudumisha amani ambayo imekuwa ikitetereka sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya kumthamini na kumuenzi mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Maisha ya kiroho ni jukwaa makini kwa waamini wa dini mbali mbali kuweza kukutana na kujadiliana hatima ya maisha yao kwa siku za usoni. Hiki ndicho kiini cha majadiliano ya kidini na kiekumene, kama alivyobainisha baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati viongozi wa dini na madhehebu mbali mbali walipokutana mjini Assis kusali kwa pamoja, kama kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka 25 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili alipowakutanisha viongozi wa dini na madhehebu mbali mbali kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani.

Ni changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali kutafuta ukweli, mafao ya wengi, utunzaji wa mazingira na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na Muumba wake kama mwanzo wa majadiliano ya kweli. Kwa kudumisha mambo haya, taraibu binadamu anaanza kujifunza kujenga na kuimarisha utamaduni wa amani inayomjumuisha mtu mzima: kiroho na kimwili.

Wajenzi wa amani hawana budi kulinda, kudumisha na kutetea utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; kwa kutafuta kilicho cha chema na cha kweli kwa ajili ya wengi. Kumbe, anasema Askofu mkuu Giovanni Angelo Becciu.

Akichangia mada kwenye Semina hii, Bwana Michel Roy, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na mikakati endelevu ya maendeleo ya mwanadamu, ili kuiwezesha Jamii kuishi katika misingi ya udugu, haki, amani na maelewano. Papa Paulo wa sita, alikwisha wahi kusema kwamba, amani ni jina jipya la maendeleo ya mwanadamu, pasi na amani, hakuna maendeleo ya kweli.

Athari za myumbo wa uchumi kimataifa tangu mwaka 2008 ni matokeo ya ubinafsi, uchoyo na uchu wa mali na madaraka; mambo yanayomwangalia mwanadamu na Muumba wake kwa jicho la makengeza! Haya ni matokeo ya kumong’onyoka kwa tunu msingi za kimaadili na utu wema! Ni ubinafsi unaomfanya mtu kujifunga katika undani wake na kutoona umuhimu wa kushirikishana na kusaidiana kiasi cha kutoweza kujenga Jumuiya inayowajibika na kusumbukiana. Watu wanajibidisha kutafuta mali na utajiri wa haraka haraka, kiasi hata cha kubeza utu na heshima ya binadamu.

Changamoto iliyoko mbele ya Jumuiya ya Kimataifa kwa sas ana kufanya mabadiliko ya dhati, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu. Mikakati na sera za maendeleo na uchumi, zijitahidi kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili; maskini na wanyonge wakipewa umuhimu wa pekee. Lakini kwa bahati mbaya, mikakati na sera nyingi za maendeleo zimepelekea mamillioni ya watu kujikuta hawana tena fursa za ajira, wakiteseka na kuranda randa mitaani kama dala dala isiyokuwa na abiria!

Maendeleo ya Jamii, utu na heshima ya mtu; tunu bora za maisha ya kifamilia na Jamii katika ujumla wake ni mambo ambayo kwa hakika yanapaswa kufanyia kazi, ili kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu. Ikumbukwe kwamba, mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Binadamu ni chemchemi ya maisha na upendo wa dhati.

Jamii anasema Michel Roy, haina budi kujenga mazingira bora yatakayosaidia mchakato wa maendeleo endelevu na ukuaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili; Familia na Jamii kwa ujumla wake. Ulimwengu una haja ya kuwa na tunu msingi za rejea sanjari na udhbiti wa soko huria mintarafu kanuni na maadili ya kazi.

Kwa maneno machache anasema Bwana Michel Roy, Katibu mkuu wa Caritas Internatinalis kwamba, mwanadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati mbali mbali ya maendeleo endelevu!








All the contents on this site are copyrighted ©.