2013-02-28 09:14:19

Baraza la Makanisa Ulimwenguni lina mshukuru Papa Benedikto XVI


Dr. OLav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, amemwandikia barua ya shukrani Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kumshukuru kutokana na mchango wake mkubwa katika kukuza na kukoleza majadiliano ya kiekumene miongoni mwa wafuasi wa Kristo. Baraza la Makanisa linamtakia kila la kheri katika maisha yake mapya ya sala na tafakari ya kina.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, tangu mwaka 1971 akiwa Jaalim wa Taalimungu, alitoa mchango mkubwa katika majadiliano ya kiekumene, ari ambayo ameiendeleza kwa kasi mpya hata baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki katika kipindi cha miaka minane. Umoja wa Kanisa unaofumbata pia umoja wa Familia ya binadamu anasema, Dr. Tveit.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linamshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa mchango wake mkubwa wa hali na mali katika kuhimiza majadiliano ya kiekumene, kwa kukazia zaidi ushuhuda wa pamoja katika kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, utu na maadili mema sanjari na kujenga misingi ya amani na utulivu, kama ilivyojionesha wakati wa Kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka 25 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alipoitisha mkutano wa viongozi wa kidini kwa ajili ya kuombea amani duniani Mjini Assisi, Italia, kunako mwaka 2011. Mazungumzo ya viongozi hawa wawili kwa wakati huo, ilikuwa ni fursa ya kukuza na kudumisha umoja na mshikamano katika imani.







All the contents on this site are copyrighted ©.