Baadhi ya waamini wa Kanisa Katoliki China wanamshukuru Baba Mtakatifu Benedikto XVI
Baadhi ya Waamini wa Kanisa Katoliki nchini China wamemwandikia Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita, barua ya shukrani na kumwomba katika sala na tafakari zake asiwasahau
katika hija ya maisha yao ya kiiimani. Wanasema, walitamani kuona siku moja, anatembelea
China ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani wanaoendelea kuteseka kwa ajili ya
Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Waamini nchini China wanatambua na kuthamini
mchango wake uliopania kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo na kwamba,
alionesha upendo mkubwa kwa wananchi wa China tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa.
Amekuwa ni kielelezo cha majadiliano ya kina miongoni mwa wananchi wa China ili kujenga
na kuimarisha umoja na mshikamano.
Katika shida na mahangaiko ya wananchi
wa China, ameonesha mshikamano na upendo wa kibaba! Wanamkumbuka kwa kuruhusu kuchapishwa
kwa Misale ya Waamini kwa Lugha ya Kichina ambao kwa sasa ni msaada mkubwa katika
Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Wanaikumbuka ile barua aliyowaandikia kuwatia moyo
kusonga mbele katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa.