2013-02-27 09:25:50

Siku ya 8 Kimataifa kuadhimishwa kuanzia tarehe 22 - 27 Septemba 2015, huko Philadelphia, USA!


Baraza la Kipapa la Familia linatangaza kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa yatakayofanyika mjini Philadelphia, Marekani, yatafanyika kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 27 Septemba 2015. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa yatafanyika nchini Marekani, baada ya Maadhimisho haya kufanyika Jimbo kuu la Milano, Kaskazini mwa Italia, kunako mwaka 2012 na kuhudhuriwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Akizungumzia kuhusu Maadhimisho haya, Askofu mkuu Charles Chaput wa Jimbo kuu la Philadelphia, Marekani anasema, ni neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu si tu kwa ajili ya Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Marekani, bali pia ni tukio linalowagusa watu wote wenye mapenzi mema ndani na nje ya Marekani. Ni tukio linalohitaji utulivu na mipango kamambe, kwani ndani mwake kuna nguvu inayoweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii kwa ujumla wake.

Kila Adhimisho la Siku ya Familia Kimataifa, linaongozwa na kauli mbiu, kama kielelezo cha Habari Njema ya Wokovu kwa Familia ya Binadamu. Ni kauli inayofumbata kwa namna ya pekee, tunu msingi za maisha ya Kiinjili na zile za Kijamii. Tema kwa Mwaka 2015 itachaguliwa na Baba Mtakatifu Mpya. Viongozi wa Serikali mjini Philadelphia wanaonesha utashi wa kushirikiana na Kanisa ili kuweza kufanikisha Maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa.

Viongozi hao wanatambua na kuheshimu tunu msingi za maisha na utume wa Familia katika Jamii. Wanawakaribisha kwa mikono miwili wale wote watakaoshiriki katika maandalizi na hatimaye, Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa huko Philadelphia, nchini Marekani. Tangu mwaka 1994, Jumuiya ya Kimataifa ilipotangaza Mwaka wa Familia Kimataifa, Baraza la Kipapa la Familia limekuwa na dhamana ya kuandaa Siku za Familia Kimataifa kwa kushirikiana na Majimbo yanayoteuliwa na Baba Mtakatifu kuwa mwenyeji wa Maadhimisho hayo!

Itakumbukwa kwamba, kwa mara ya kwanza Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa yalifanyika mjini Roma kunako Mwaka 1994; Rio de Janeiro, Mwaka 1997, Roma ikawa ni mwenyeji wa Maadhimisho haya wakati wa Jubilee ya miaka 2000 ya Ukristo, hapo Mwaka 2000. Jimbo kuu la Manila, Ufilippini likapewa dhamana hii kunako mwaka 2003; Likafuatia Jimbo kuu la Valencia, Hispania kwa Mwaka 2006, Mexico, 2009 na Jimbo kuu la Milani, hapo mwaka 2012. Kwa mwaka 2015, Jimbo kuu la Philadelphia litakuwa ni mwenyeji wa Maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa.







All the contents on this site are copyrighted ©.