2013-02-27 07:53:04

Mshikamano wa: haki, amani na upendo kwa Waamini wanaoishi katika Nchi Takatifu


Maadhimisho ya Mwaka wa Imani sanjari na kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni mwaliko na changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha mshikamano wa upendo kwa waamini wanaoishi katika Nchi Takatifu, ambao miaka nenda miaka rudi, wameendelea kulinda na kutunza maeneo ya imani. Nchi Takatifu inaonesha ile kiu ya haki, utu na heshima, ili kwa pamoja Jamii iweze kuwajibika kuwalinda na kuwatunza wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili kwa pamoja waweze kusimama kidete kutetea mafao ya wengi pamoja na kuwajibika barabara

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki katika barua yake kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, sehemu mbali mbali za dunia linasema, kuna watu wanaendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini kwa kukosa mahitaji msingi ya maisha kutokana na ubinafsi uliokithiri. Kila mtu anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wake, daima Jamii ikijikita kutafuta mafao ya wengi pamoja na amani ya kudumu. Binadamu anatambua kwamba, hatima ya maisha yake hapa duniani ni kutaka kuungana na Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo imani inayoliongoza Kanisa, kwa kujitahidi kutafuta umoja na mshikamano na Kristo.

Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki anasema kwamba, kunako mwaka 1964, Papa Paulo wa sita katika hija yake ya kichungaji katika Nchi Takatifu; baadaye Mtumishi wa Mungu Yohane Paulo wa pili, alisema kwamba, hija yake ambayo ilikuwa ni zawadi kubwa katika Maadhimisho ya Jubilee kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo ilipania kujenga na kuimarisha umoja, udugu na amani, kwa kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa Waamini wanaoishi katika Nchi Takatifu, ili hatimaye, kuweza kupata suluhu ya migogoro na kinzani zinazojitokeza katika Nchi Takatifu.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, mara baada ya kurejea mjini Vatican baada ya hija yake ya kichungaji aliwaombea Wakristo wanaoishi Mashariki ya kati, ili kwa nguvu ya Roho Mtakatifu waweze kudumu katika uaminifu. Ili kuonesha ukaribu wake na Wakristo wanaoishi Mashariki ya Kati, ambao wanakumbana na madhulumu pamoja na changamoto mbali mbali, amewadhaminisha kuandika tafakari ya Ibada ya Njia ya Msalaba, Ijumaa Kuu, kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma. Sehemu hii inahitaji umoja na mshikamano katika fadhila ya imani.

Waamini wanachangamotishwa kuonesha moyo wa mshikamano kwa kuchangia kwa hali na mali utunzaji wa maeneo matakatifu, tukio ambalo linafanywa na Mama Kanisa, katika Ibada ya Ijumaa kuu. Msaada huu unalenga kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu unaofanywa na Kanisa mahalia katika sekta mbali mbali za maisha. Mchango huu pia ni chanzo cha pato kwa Familia nyingi zinazokabiliana na hali ngumu ya maisha, ili kuweza kuwahudumia: wagonjwa, wazee, watoto yatima na walemavu.

Mshikamano kutoka kwa waamini sehemu mbali mbali za dunia, imekuwa pia ni fursa ya kutoa ajira kwa vijana ili kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Lengo la mchango huu ni kujenga na kuimarisha uhuru wa kidini; majadiliano ya kidini na kiekumene pamoja na kuwasaidia Wakristo ili waweze kuendelea kubaki katika maeneo yao badala ya kukimbilia sehemu nyingine. Hapa ni kielelezo cha mateso na mahangaiko ya binadamu, lakini mahali ambapo pia Mwenyezi Mungu anatukuzwa na mwanadamu anatakatifuzwa. Baraza la Kipapa linawahimiza waamini kuchagia kwa hali na mali katika kuenzi shughuli za imani na maendeleo Nchi Takatifu.








All the contents on this site are copyrighted ©.