Mwongozo kuhusu muundo, utaratibu wa kupata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba katika Wilaya
(Mamlaka za Serikali za Mitaa) na uendeshaji wake!
1.0. UTANGULIZI Kwa
mujibu wa Kifungu cha 18 (3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, Tume
inawajibu wa kuunda Mabaraza ya Katiba kwa ajili ya kupitia na kutoa maoni juu ya
Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume. Muundo wa Mabaraza ya Katiba unapaswa kuzingatia
mgawanyiko wa kijiografia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mabaraza ya Katiba yatawashirikisha
na kuwakutanisha wawakilishi kutoka makundi mbalimbali ya wananchi katika jamii kwa
lengo la kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba. Aidha, kifungu cha 17 (8) kinaeleza
kuwa, isipokuwa kama mazingira yatahitaji vinginevyo, Tume itabuni utaratibu unaofanana
ambao utatumika kila upande wa Muungano. Kifungu cha 18 (6) kinaeleza aina nyingine
ya Mabaraza ya Katiba. Kwa mujibu wa Kifungu kidogo cha (6), Tume inaweza kuruhusu
Asasi, Taasisi au Makundi ya watu kuandaa mikutano kwa ajili ya kutoa fursa kwa wanachama
wake kutoa maoni yao juu ya Rasimu ya Katiba na kisha kuwasilisha maoni hayo kwa Tume.
Kwa Msingi huo, Tume imeamua kuwa Mabaraza ya Katiba yatakuwa katika makundi mawili
yafuatayo:- 1.1 Mabaraza ambayo Tume itayasimamia na kukusanya Maoni (Mabaraza
ya Katiba ya Wilaya – Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa).
1.2
Mabaraza ambayo Tume haitayasimamia. Mabaraza hayo yatajisimamia yenyewe na kukusanya
maoni yatakayowasilishwa kwenye Tume kwa mujibu wa maelekezo. (Mabaraza ya Katiba
ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu). Mwongozo huu unaainisha Muundo, Utaratibu
wa kuwapata Wajumbe na Utaratibu wa Uendeshaji wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi
ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yatakayoendeshwa na kusimamiwa na Tume. 2.0.
MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA NGAZI YA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA Kwa kuzingatia
mgawanyiko wa kijiografia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya – Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa yataundwa kwenye kila Mamlaka ya Serikali
za Mitaa katika ngazi ya Halmashauri za Jiji, Manispaa, Mji, Wilaya na Mabaraza ya
Miji. Kwa upande wa Tanzania Bara, Katika Mikoa yote ngazi ya kupata wajumbe wa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) itakuwa ni Ngazi ya Kata.
Wajumbe watapigiwa kura za kupendekezwa kwenye ngazi za Kijiji/Mitaa na kuchaguliwa
kwenye ngazi ya Kata. Kwa upande wa Zanzibar, Katika Mikoa yote ngazi ya kupata
wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) itakuwa ni
Shehia. Wajumbe watapigiwa kura kwenye ngazi za Shehia. Muundo na utaratibu huu
umezingatia changamoto mbalimbali zikiwemo; ukubwa wa Mabaraza ya Katiba, utaratibu
wa kuwapata wajumbe, ufanisi katika uendeshaji wa Mabaraza ya Katiba, gharama ya kufanikisha
shughuli ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, na
tofauti ya Mfumo wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara na Zanzibar. Kutokana na changamoto
hizo, utaratibu wa kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya haufanani kwa
pande zote za Muungano. 3.0. WAJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA NGAZI YA
MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA
3.1 Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba.
Mabaraza ya Katiba katika ngazi ya Halmashauri za Jiji, Manispaa, Mji, Wilaya
na Mabaraza ya Miji yataundwa na Wajumbe wafuatao:-
3.1.1. Kwa Tanzania Bara.
3.1.1.1 Wajumbe wanne kutoka kila Kata watachaguliwa kwautaratibu utakaofafanuliwa
na Mwongozo huu. 3.1.1.2 Wajumbe wanane kutoka kila Kata kwa Mkoa wa Dar
es Salaam.
3.1.2. Kwa Zanzibar. 3.1.2.1. Wajumbe watatu kutoka kila
Shehia watachaguliwa kwa utaratibu utakaofafanuliwa na Mwongozo huu.
3.1.3.
Kwa pande zote za Muungano.
3.1.3.1. Madiwani wa kuchaguliwa kwenye Kata
/ Wadi.
3.1.3.2. Madiwani wa Viti Maalum.
3.1.3.3. Madiwani
wa kuteuliwa na Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kwa pande zote za Muungano
[Madiwani waliopo kazini kwa sasa].
3.2 Ngazi ya Msingi ya kuwapata
Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba
3.2.1. Kwa upande wa Tanzania Bara Kwa
Mikoa yote ya Tanzania Bara, ngazi ya msingi ya kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba
itakuwa Kata.
3.2.2. Kwa upande wa Zanzibar Kwa Mikoa yote ya Zanzibar,
ngazi ya msingi ya kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba itakuwa Shehia.
3.3
Idadi ya Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
Idadi
ya Wajumbe itakuwa kama ifuatavyo:-
3.3.1. Kwa Tanzania Bara, idadi ya Mabaraza
ya Katiba yatakayoendeshwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni 163 ambapo kila
Mamlaka moja ya Serikali za Mitaa ngazi ya Wilaya itakuwa na Baraza moja la Katiba
ukiondoa Mkoa wa Dar es Salaam ambapo kila Halmashauri itakuwa na Mabaraza mawili
ya Katiba. Hivyo, jumla ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali
za Mitaa itakuwa 163 (zipo Mamlaka za Serikali za Mitaa 160).
3.3.2. Katika
Mikoa 24 ya Tanzania Bara, kila kata itawakilishwa na Wajumbe wanne (4) ambao wataungana
na Madiwani wa Kata na Viti Maalum. Idadi ya Kata ni 3,339 ukiondoa kata 90 za Mkoa
wa Dar es Salaam, zinabaki kata 3,249 [utaratibu wa kuwapata wajumbe kwa Mkoa wa Dar
es Salaam ni tofauti na Mikoa mingine ya Tanzania Bara na umefafanuliwa katika aya
ya 3.3.3]. Hivyo, Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kutoka kwenye Kata zote
isipokuwa kata 90 za Mkoa wa Dar es Salaam, watakuwa 12,996 na idadi ya Madiwani wote
ni 4,453.
3.3.3. Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, wenye Kata 90 utawakilishwa na
Wajumbe wanane (8) kutoka kila Kata. Kwa hiyo, idadi ya Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba
ya Wilaya kutoka Mkoa Dar es Salaam Watakuwa 720 watakaoungana na Wajumbe wengine
kama ilivyofafanuliwa kwenye aya ya 3.3.2.
Jumla ya Wajumbe wote wa Mabaraza
ya Katiba kwa Tanzania Bara watakuwa 18,169 kwa mchanganuo ufuatao:-
3.3.3.1.
Idadi ya Wajumbe 4 kutoka kila Kata 12,996
3.3.3.2.
Idadi ya Wajumbe 8 kutoka Kata za Mkoa wa Dar es
salaam 720
3.3.3.3.
Idadi ya Madiwani wote ni: 4,453
18,169
JUMLA:
3.3.4. Kwa upande wa Zanzibar, idadi ya Mabaraza ya Katiba yatakayoendeshwa
katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni 13 ambapo kila Mamlaka moja ya Serikali za
Mitaa itakuwa na Baraza moja la Katiba (zipo Mamlaka za Serikali za Mitaa 13).
3.3.5.
Katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 13 za Zanzibar, kila Shehia itawakilishwa na Wajumbe
watatu (3) ambao wataungana na Madiwani wa Wadi, Viti Maalum, na Wakuteuliwa waliopo
kazini kwa sasa. Idadi ya Shehia ni 335. Hivyo, Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya
kutoka kwenye Shehia zote watakuwa 1,005 na idadi ya Madiwani wote ni 193.
Jumla
ya Wajumbe wote wa Mabaraza ya Katiba kwa Zanzibar watakuwa 1,198 kwa mchanganuo ufuatao:-
3.3.5.1.Idadi
ya Wajumbe kutoka kila Shehia: 1,005
3.3.5.2.Idadi ya Madiwani Wote ni:
193
1,198
JUMLA
Mchanganuo
wa idadi ya Wajumbe kwa kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni kama ilivyo kwenye Jedwali
“1” kwa upande wa Tanzania Bara na Jedwali “2” kwa Zanzibar.
4.0. SIFA
ZA WATAKAOCHAGULIWA KUWA WAJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA NGAZI YA MAMLAKA
ZA SERIKALI ZA MITAA.
Wajumbe wanne kutoka kila Kata kwa Tanzania Bara na wanane
kutoka kila Kata katika Mkoa wa Dar es Salaam na Wajumbe watatu kutoka kila Shehia
kwa Zanzibar wanapaswa kuwa na sifa zifuatazo kwa pamoja:-
4.1 Awe
ni Raia wa Tanzania. 4.2 Awe na umri wa miaka 18 au zaidi. 4.3
Awe na uwezo wa kusoma na kuandika. 4.4 Awe ni mkazi wa kudumu wa Kijiji/
Mtaa / Shehia husika. 4.5 Awe ni Mtu mwenye hekima, busara na uadilifu. 4.6
Awe ni Mtu mwenye uwezo wa kujieleza na kupambanua mambo.
5.0. MAMBO YA KUZINGATIWA Licha
ya sifa zilizotajwa katika aya ya 4.0., utaratibu wa kuwapata Wajumbe kwa Tanzania
Bara na Zanzibar uzingatie mambo yafuatayo:- 5.1 Uwakilishi wa watu
wazima. 5.2 Uwakilishi wa wanawake. 5.3 Uwakilishi wa
vijana, yaani kati ya miaka 18 hadi 35. 5.4 Jiografia ya Kata/ Wadi
/ Kijiji / Mtaa / Shehia husika.
6.0. UTARATIBU WA KUWAPATA WAJUMBE KWENYE
MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA NGAZI YA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA
6.1
Kwa upande wa Tanzania Bara utaratibu utakuwa kama ifuatavyo:-
Kwa Mikoa yote
isipokuwa Mkoa wa Dar es Salaam.
6.1.1. Kwa kuzingatia sifa zilizoainishwa
kwenye aya za 4.0 na 5.0, kila Mwananchi wa Kijiji / Mtaa husika anayependa kuwa Mjumbe
wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa atawasilisha
jina lake kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji / Mtaa. Uwasilishaji huo uambatane na taarifa
zifuatazo:- 6.1.1.1. Majina kamili ya mwombaji. 6.1.1.2. Jinsi yake. 6.1.1.3.
Umri wake. 6.1.1.4. Elimu yake. 6.1.1.5. Kazi yake. 6.1.1.6.
Sehemu anayoishi katika Kijiji / Mtaa husika.
6.1.2. Wakati wa uwasilishaji
wa jina, kila mwananchi anayependa kuwa Mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya, atawasilisha
nakala mbili za barua kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji / Mtaa. Nakala moja ibaki kwa Afisa
Mtendaji wa Kijiji / Mtaa; na nakala ya pili iwekwe Mhuri na saini ya Afisa Mtendaji
wa Kijiji / Mtaa. Nakala hiyo abaki nayo mwanachi husika kwa uthibitisho kuwa barua
yake ilipokelewa.
6.1.3. Orodha ya majina ya Wananchi wote wanaotaka kuwa
Wajumbe yatabandikwa kwenye maeneo ya wazi / matangazo ya kila Ofisi za Kijiji / Mtaa
siku saba (7) kabla ya Mkutano ili wananchi wapate fursa ya kuyapitia na kujiridhisha
kama walioomba wana sifa zilizoanishwa kwenye aya za 4.0 na 5.0. 6.1.4. Afisa
Mtendaji wa Kijiji / Mtaa ataitisha Mkutano Mkuu Maalum wa Kijiji / Mtaa ambao utakuwa
na agenda moja tu ya kuwapendekeza kwa kuwapigia kura watu wanne ambao majina yao
yatawasilishwa kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata. Mkutano huu utaendeshwa na Mwenyekiti
wa Kijiji / Mtaa, ambapo Afisa Mtendaji wa Kijiji / Mtaa atakuwa Katibu wa Mkutano
huo na ndiye atakayewasilisha majina ya wananchi wote walioomba kuingia kwenye Baraza
la Katiba la Wilaya.
6.1.5. Kwa kuzingatia Sifa zilizoainishwa katika aya
za 4.0. na 5.0, Mkutano Mkuu Maalum wa Kijiji / Mtaa utayapigia kura ya siri majina
ya wananchi walioomba kuwa Wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ngazi ya Mamlaka
za Serikali za Mitaa.
6.1.6. Utaratibu wa kupiga kura za kwenye Mkutano
Mkuu Maalum wa kuwachagua Wananchi wanne wanaopendekezwa kuwa Wajumbe wa Mabaraza
ya Katiba ya Wilaya utakuwa kama ifuatavyo:-
6.1.6.1. Kwanza, Wajumbe
wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa Kijiji / Mtaa watapiga kura ya siri ya kumchagua Mtu
mzima mmoja [anaweza kuwa mwanamke au mwanamme]. 6.1.6.2. Pili, Wajumbe wote
wa Mkutano Mkuu Maalum wa Kijiji / Mtaa watapiga kura ya siri ya kumchagua Mwanamke
mmoja. 6.1.6.3. Tatu, Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa Kijiji / Mtaa
watapiga kura ya siri ya kumchagua Kijana mmoja [anaweza kuwa Mwanamme au Mwanamke]. 6.1.6.4.
Nne, Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa Kijiji / Mtaa watapiga kura ya siri ya
kumchagua Mtu mwingine yeyote kutoka miongoni mwa Wananchi walioomba kuwa Wajumbe
wa Baraza la katiba la wilaya.
6.1.7. Orodha ya majina ya wananchi wanne
waliopigiwa kura nyingi za kupendekezwa kuwa Wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya
ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, yatabandikwa kwenye maeneo ya wazi/ matangazo
ya kila Ofisi ya Serikali ya Kijiji / Mtaa.
6.1.8. Majina ya watu wanne yatakayokuwa
yamepata kura nyingi kuliko mengine yatawasilishwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji / Mtaa
kwa Afisa Mtendaji wa Kata yakiwa yameambatanishwa na Muhtasari wa Mkutano Mkuu Maalum
wa Kijiji / Mtaa uliosainiwa na Mwenyekiti wa Kijiji /Mtaa pamoja na orodha ya wananchi
waliohudhuria.
6.1.9. Afisa Mtendaji wa Kata baada ya kupokea majina yaliyopendekezwa
kutoka kwenye Mikutano Mikuu Maalum ya Vijiji / Mitaa ya Kata husika, ataitisha Kikao
Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata, ambacho kwa kuzingatia sifa zilizoainishwa
kwenye aya za 4.0 na 5.0 kitachagua majina manne kwa kura ya siri kwa utaratibu ufuatao:-
6.1.9.1.
Kwanza, Wajumbe wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watapiga kura ya siri ya kumchagua
Mtu mzima mmoja [anaweza kuwa mwanamke au Mwanamme].
6.1.9.2. Pili, Wajumbe
wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watapiga kura ya siri ya kumchagua Mwanamke mmoja.
6.1.9.3.
Tatu, Wajumbe wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watapiga kura ya siri ya kumchagua
Kijana mmoja [anaweza kuwa Mwanamme au Mwanamke].
6.1.9.4. Nne, Wajumbe
wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watapiga kura ya siri ya kumchagua Mtu mwingine
yeyote kutoka miongoni mwa wananchi walioomba kuwa Wajumbe wa Baraza la Katiba la
Wilaya.
6.1.10. Jina la Mwananchi atakayekuwa amepata kura nyingi kutoka
kila kundi [Mtu mzima, Mwanamke, Kijana na Mtu mwingine yeyote] yatawasilishwa kwa
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa yakiwa na Muhtasari uliosainiwa na Mwenyekiti
na Katibu wa Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata kilichoyapigia kura majina
hayo pamoja na orodha ya Wajumbe waliohudhuria.
6.1.11. Mkurugenzi wa Mamlaka
ya Serikali za Mitaa kwa kuzingatia sifa na utaratibu ulioainishwa kwenye aya za 4.0
na 5.0, atawasilisha majina kwa Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa Uteuzi.
6.1.12.
Endapo Diwani wa kata ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata hatakuwepo
[Kwa sababu zozote ikiwa ni pamoja na kuwa safarini kwa kipindi ambacho Mabaraza ya
Katiba yatafanyika, kuwa mgonjwa na kutoweza kutekeleza majukumu ya Udiwani, Kifo
au sababu nyingine], utaratibu wa kawaida wa kumpata mwenyekiti wa kikao cha Kamati
ya Maendeleo ya Kata wakati Diwani hayupo utatumika, ambapo Mwenyekiti wa Kijiji/Mtaa
atakayependekezwa na Wajumbe wenzake wa Kamati ya Maendeleo ya Kata kuendesha Kikao
hicho ndiye atawakilisha kata badala ya Diwani.
6.2 Kwa Mkoa wa Dar
es Salaam utaratibu utakuwa kama ifuatavyo:-
6.2.1. Kwa kuzingatia sifa zilizoainishwa
kwenye aya za 4.0 na 5.0, kila Mwananchi wa Mtaa husika anayependa kuwa Mjumbe wa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa atawasilisha jina
lake kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa. Uwasilishaji huo uambatane na taarifa zifuatazo:-
6.2.1.1.
Majina kamili ya mwombaji. 6.2.1.2. Jinsi yake. 6.2.1.3. Umri wake. 6.2.1.4.
Elimu yake. 6.2.1.5. Kazi yake. 6.2.1.6. Sehemu anayoishi katika Mtaa
husika.
6.2.2. Wakati wa uwasilishaji wa jina, kila mwananchi anayependa
kuwa Mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya, atawasilisha nakala mbili za barua kwa
Afisa Mtendaji wa Mtaa. Nakala moja ibaki kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa; na nakala ya
pili iwekwe Mhuri na saini ya Afisa Mtendaji wa Mtaa. Nakala hiyo abaki nayo mwanachi
husika kwa uthibitisho kuwa barua yake ilipokelewa.
6.2.3. Orodha ya majina
ya Wananchi wote wanaotaka kuwa wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ngazi ya Mamlaka
za Serikali za Mitaa, itawekwa kwenye maeneo ya wazi / matangazo ya Ofisi za Mtaa
kwa siku saba (7) kabla ya Mkutano ili wananchi wa Mtaa husika wapate fursa ya kuyapitia
na kujiridhisha kama walioomba wana sifa zilizoanishwa kwenye aya za 4.0 na 5.0.
6.2.4.
Afisa Mtendaji wa Mtaa ataitisha Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa ambao utakuwa na agenda
moja tu kuwapendekeza kwa kuwapigia kura ya siri watu Wanane watakaokuwa wajumbe wa
Mabaraza ya katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
6.2.5.
Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa wa kuwachagua wananchi wanane (8) kuwa Wajumbe wa Mabaraza
ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa utaendeshwa na Mwenyekiti
wa Mtaa ambapo Afisa Mtendaji wa Mtaa atakuwa Katibu, na ndiye atakayewasilisha majina
ya wananchi wote kwenye Mkutano huo walioomba kuingia kwenye Baraza la Katiba la Wilaya.
6.2.6.
Utaratibu wa kupiga kura za kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa wa kuwachagua Wananchi
wanane wanaopendekezwa kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya utakuwa kama ifuatavyo:-
6.2.6.1.
Kwanza, Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa watapiga kura ya siri ya kuwachagua
Watu Wazima Wawili [wanaweza kuwa Wanawake au Wanaume].
6.2.6.2. Pili,
Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa watapiga kura ya siri ya kuwachagua Wanawake
wawili.
6.2.6.3. Tatu, Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa watapiga
kura ya siri ya kuwachagua Vijana wawili [wanaweza kuwa Wanaume au Wanawake].
6.2.6.4.
Nne, Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa watapiga kura za siri kuwachagua
Watu wengine wawili wowote kutoka miongoni mwa majina yaliyowasilishwa kwenye Mkutano
Mkuu Maalum wa Mtaa.
6.2.7. Orodha ya majina ya Wananchi wanane waliopigiwa
kura nyingi za kupendekezwa kuwa Wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ngazi ya Mamlaka
za Serikali za Mitaa, yatabandikwa kwenye maeneo ya wazi/ matangazo ya kila Ofisi
ya Serikali ya Mtaa.
6.2.8. Majina ya watu wanane yatakayokuwa yamepata kura
nyingi kuliko mengine, yatawasilishwa na Afisa Mtendaji wa Mtaa kwa Afisa Mtendaji
wa Kata yakiwa yameambatanishwa na Muhtasari wa Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa uliosainiwa
na Mwenyekiti wa Mtaa pamoja na orodha ya Wananchi waliohudhuria.
6.2.9.
Afisa Mtendaji wa Kata baada ya kupokea majina yaliyopendekezwa kutoka kwenye Mikutano
Mikuu Maalum ya Mitaa ya Kata husika, ataitisha Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo
ya Kata, ambacho kwa kuzingatia sifa zilizoainishwa kwenye aya za 4.0 na 5.0 kitachagua
majina manane kwa kura ya siri kwa utaratibu ufuatao:-
6.2.9.1.
Kwanza, Wajumbe wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watapiga kura ya siri ya kuwachagua
Watu wazima wawili [wanaweza kuwa Wanawake au Wanaume].
6.2.9.2. Pili,
Wajumbe wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watapiga kura ya siri kuwachagua Wanawake
wawili. 6.2.9.3. Tatu, Wajumbe wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watapiga
kura ya siri kuwachagua Vijana wawili [wanaweza kuwa wanaume au wanawake].
6.2.9.4.
Nne, Wajumbe wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watapiga kura ya siri kuwachagua
watu wawili wengine wowote, kutoka miongoni mwa majina yaliyowasilishwa kwenye Kikao
Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata.
6.2.10. Majina
ya Wananchi watakaokuwa wamepata kura nyingi kutoka kila kundi [Watu wazima wawili,
Wanawake wawili, Vijana wawili na Watu wawili wengine] yatawasilishwa kwa Mkurugenzi
wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa yakiwa na Muhtasari uliosainiwa na Mwenyekiti na Katibu
wa Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata, kilichoyapigia kura majina hayo pamoja
na orodha ya Wajumbe waliohudhuria.
6.2.11. Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali
za Mitaa kwa kuzingatia sifa na utaratibu ulioainishwa kwenye aya za 4.0 na 5.0, atawasilisha
majina kwa Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa Uteuzi.
6.2.12. Endapo
Diwani wa Kata ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata hatakuwepo [Kwa
sababu zozote ikiwa ni pamoja na kuwa safarini kwa kipindi ambacho Mabaraza ya Katiba
yatafanyika, kuwa mgonjwa na kutoweza kutekeleza majukumu ya Udiwani, kifo au sababu
nyingine], utaratibu wa kawaida wa kumpata Mwenyekiti wa kikao cha Kamati ya Maendeleo
ya Kata wakati Diwani hayupo utatumika, ambapo Mwenyekiti wa Mtaa atakayependekezwa
na Wajumbe wenzake wa Kamati ya Maendeleo ya Kata kuendesha Kikao hicho ndiye atawakilisha
kata badala ya Diwani.
6.3 Kwa upande wa Zanzibar utaratibu utakuwa
kama ifuatavyo:-
6.3.1. Kwa kuzingatia sifa zilizoainishwa kwenye aya za
4.0 na 5.0, kila Mwananchi Mkaazi wa Shehia husika anayependa kuwa mjumbe wa Mabaraza
ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa atawasilisha jina lake kwa
Sheha. Uwasilishaji huo uambatane na taarifa zifuatazo:-
6.3.1.1. Majina
kamili ya mwombaji. 6.3.1.2. Jinsi yake. 6.3.1.3. Umri wake. 6.3.1.4.
Elimu yake. 6.3.1.5. Kazi yake. 6.3.1.6. Sehemu anayoishi katika Shehia
husika.
6.3.2. Wakati wa uwasilishaji wa jina, kila Mwananchi anayependa
kuwa Mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya, atawasilisha nakala mbili za barua kwa
Sheha. Nakala moja ibaki kwa Sheha; na nakala ya pili iwekwe Mhuri na saini ya Sheha.
Nakala hiyo abaki nayo Mwanachi husika kwa uthibitisho kuwa barua yake ilipokelewa.
6.3.3.
Orodha ya majina ya Wananchi wote walioomba kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yatabandikwa kwenye maeneo ya wazi (mfano
Skuli) / matangazo katika Shehia husika siku saba (7) kabla ya Mkutano ili Wananchi
wapate fursa ya kuyapitia na kujiridhisha kama walioomba wana sifa zilizoanishwa kwenye
aya za 4.0 na 5.0.
6.3.4. Sheha ataitisha Mkutano wa Shehia husika ambao
utakuwa na agenda moja tu ya kuwapigia kura ya siri watu watatu [3] ambao majina yao
yatawasilishwa kwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Katibu wa Halmashauri Mji/ Wilaya
ambapo Shehia hiyo ipo.
6.3.5. Mkutano wa Shehia utachagua Mwenyekiti na
Katibu wa Mkutano huo kutoka miongoni mwa Wananchi waliohudhuria Mkutano. Katibu ndiye
atakayewasilisha kwenye Mkutano majina ya Wananchi wote walioomba kuwa Wajumbe wa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
6.3.6.
Mwenyekiti na Katibu wa Mkutano wa Shehia watakaochaguliwa sharti wawe na sifa kama
za Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba zilivyoainishwa katika aya ya 4.0.
6.3.7.
Utaratibu wa kupiga kura kwenye Mkutano wa Shehia wa kuwachagua Wananchi watatu kuwa
Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya utakuwa kama ifuatavyo:-
6.3.7.1.
Kwanza, Wananchi wote waliohudhuria Mkutano wa Shehia watapiga kura ya siri ya kumchagua
Mtu mzima mmoja [anaweza kuwa Mwanamke au Mwanamme].
6.3.7.2. Pili, Wananchi
wote waliohudhuria Mkutano wa Shehia watapiga kura ya siri ya kumchagua Mwanamke mmoja.
6.3.7.3.
Tatu, Wananchi wote waliohudhuria Mkutano wa Shehia watapiga kura ya siri ya kumchagua
Kijana mmoja [anaweza kuwa Mwanamme au Mwanamke].
6.3.8. Matokeo ya upigaji
kura wa siri yatatangazwa kwenye Mkutano baada ya mchakato wa kupiga kura kukamilika
na kuwekwa kwenye maeneo ya wazi / matangazo katika Shehia husika.
6.3.9.
Katibu wa Mkutano wa Shehia, atawasilisha majina ya watu watatu (3) waliochaguliwa
katika Mikutano ya Shehia kwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Katibu wa Halmashauri
ya Mji / Wilaya ambapo Shehia hiyo ipo katika muda wa siku moja tangu Mkutano ulipofanyika.
Mawasilisho hayo yaambatane na muhtasari wa Mkutano uliotiwa saini na Mwenyekiti na
Katibu pamoja na orodha ya majina ya wananchi waliohudhuria.
6.3.10. Mkurugenzi
wa Baraza la Manispaa, Katibu wa Halmashauri Mji/ Wilaya kwa kuzingatia sifa na utaratibu
ulioainishwa kwenye aya za 4.0 na 5.0, atawasilisha majina kwa Katibu wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba kwa uteuzi.
Baada ya kupokea orodha ya majina ya watu waliochaguliwa
kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa
kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, Katibu atatoa barua rasmi za kuwateua Wajumbe wa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
7.0. TARATIBU
ZA KUFANYA MIKUTANO YA KUWAPATA WAJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA.
Ili
kuendana na muda wa kuwapata Wajumbe na kufanyika kwa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya
ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa pamoja na maandalizi yote muhimu, vikao vya
kupendekeza majina na kufanya uchaguzi vitafanyika kwa utaratibu ufuatao:-
7.1
Wananchi wanaopenda kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya wawasilishe majina
yao kwa Maafisa Watendaji wa Vijiji / Mitaa kwa Tanzania Bara na kwa Sheha kwa Zanzibar
kati ya tarehe 08 Machi, 2013 hadi 20 Machi, 2013.
7.2 Orodha ya
majina ya Wananchi wote wanaotaka kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi
ya Mamlaka za Serikali za Mitaa iwekwe kwenye maeneo ya wazi / matangazo katika Ofisi
za Vijiji / Mitaa kwa Tanzania Bara; na katika maeneo ya wazi / matangazo kwenye Shehia
husika kwa Zanzibar tarehe 22 Machi, 2013 na majina hayo yaendelee kuwepo hadi tarehe
28 Machi, 2013.
7.3 Kwa Tanzania Bara, Vikao vya Vijiji / Mitaa
vya kuwachagua kwa kuwapigia kura za siri wananchi wanne kuwa Wajumbe wa Mabaraza
ya Katiba vifanyike kati ya tarehe 30 Machi 2013 hadi 03 Aprili, 2013.
7.4
Kwa upande wa Tanzania Bara, Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata cha kuwachagua
wajumbe wanne kutoka miongoni mwa Wananchi waliopigiwa kura na Mikutano Mikuu ya Vijiji
/ Mitaa kifanyike kati ya tarehe 05 Aprili 2013 hadi 09 Aprili, 2013.
7.5
Kwa Tanzania Bara, majina ya Wajumbe wanne waliochaguliwa na Kikao Maalum cha Kamati
ya Maendeleo ya Kata, yawasilishwe kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa
husika kati ya tarehe 13 Aprili, 2013 hadi 17 Aprili, 2013.
7.6
Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, 7.6.1. Vikao vya Mitaa vya kuwapigia kura ya kuwapendekeza
wajumbe wanane wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya vifanyike kati ya tarehe 30 Machi,
2013 hadi 03 Aprili, 2013.
7.6.2. Vikao Maalum vya Kamati za Maendeleo za
Kata vya kuwachagua wajumbe wanane kutoka miongoni mwa wananchi waliopigiwa kura na
Mikutano Mikuu ya Mitaa vifanyike kati ya tarehe 05 Aprili, 2013 hadi 09 Aprili, 2013.
7.6.3.
Majina ya Wajumbe wanane waliochaguliwa na Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya
Kata, yawasilishwe kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa husika kati ya tarehe
13 Aprili 2013 hadi 17 Aprili, 2013.
7.7 Kwa Zanzibar, 7.7.1.
Vikao vya Shehia vya kuwachagua kwa kuwapigia kura za siri Wananchi watatu kuwa Wajumbe
wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya vifanyike kati ya tarehe 30 Machi, 2013 hadi 03 Aprili,
2013. 7.7.2. Majina ya Wajumbe watatu, waliochaguliwa na Mikutano ya Shehia,
yawasilishwe kwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Katibu wa Halmashauri ya Mji /
Wilaya ambapo Shehia hiyo ipo kati ya tarehe 13 Aprili 2013 hadi 17 Aprili, 2013.
Majina
ya watu wote waliochaguliwa kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, pamoja na
majina ya Madiwani wote wa Mamlaka ya Serikali za Mtaa husika yawasilishwe kwa Katibu
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kutumia Fomu maalum iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba kwa madhumuni hayo kwa njia ya nakala tete (soft Copy) na nakala mango (hard
copy) kati ya tarehe 25 Aprili 2013 hadi 30 Aprili, 2013.
8.0. MAMBO YA KUZINGATIA
KATIKA MCHAKATO WA KUWAPATA WAJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA Ni Jukumu
la Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia, kuratibu na kuhakikisha
Mikutano hiyo inafanyika.
8.1 Kwa Tanzania Bara isipokuwa kwa Mkoa
wa Dar es Salaam
8.1.1. Mikutano yote ya Vijiji / Mitaa itaendeshwa
na Wenyeviti wa Serikali za Vijiji / Mitaa na Maafisa Watendaji wa Vijiji / Mitaa
watakuwa ni Makatibu na wasimamizi wa Mikutano hiyo.
8.1.2. Mikutano
Mikuu yote ya Vijiji / Mitaa itakayoitishwa kwa lengo la kuwapigia kura ya siri watu
wanne kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya vifanyike katika tarehe moja kwenye
Vijiji / Mitaa yote iliyopo kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa husika.
8.1.3.
Vikao vyote vya Kamati za Maendeleo za Kata vitakavyokuwa na jukumu la kuwachagua
watu wanne kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali
za Mitaa vifanyike katika tarehe moja kwenye Kata zote za Mamlaka ya Serikali za Mitaa
husika.
8.1.4. Kwa Mkoa wa Dar es Salaam:
8.1.4.1. Mikutano Mikuu
yote ya Mitaa itakayoitishwa kwa lengo la kuwapigia kura watu wanane wanaopendekezwa
kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ifanyike katika tarehe moja kwenye Mitaa
yote iliyopo kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa husika.
8.1.4.2. Vikao
vyote vya Kamati za Maendeleo za Kata vitakavyokuwa na jukumu la kuwachagua watu wanane
kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa
vifanyike katika tarehe moja kwenye Kata zote za Mamlaka ya Serikali za Mitaa husika. 8.2
Kwa Zanzibar
8.2.1. Ni jukumu la Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Katibu
wa Halmashauri ya Mji / Wilaya kusimamia, kuratibu na kuhakikisha Mikutano hiyo inafanyika.
8.2.2.
Mikutano yote ya Shehia itaendeshwa na Wenyeviti na Makatibu watakaochaguliwa na Mikutano
hiyo.
8.2.3. Jukumu la Sheha ni:-
8.2.3.1. Kupokea majina ya
Wananchi wanaoomba kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
8.2.3.2.
Kubandika katika maeneo ya wazi / matangazo majina yote ya watu walioomba kuwa Wajumbe
wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
8.2.3.3. Kuitisha Mkutano wa Shehia utakaochagua
Mwenyekiti na Katibu wa Mkutano.
8.2.4. Majukumu ya Katibu wa Mkutano atakayechaguliwa:- 8.2.4.1.
Kupokea orodha ya majina ya Wananchi wote walioomba kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba
ya Wilaya kutoka kwa Sheha.
8.2.4.2. Kuwasilisha majina ya Wananchi wote
walioomba kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwenye Mkutano. 8.2.4.3.
Kuratibu mchakato wa uchaguzi kwenye Mkutano.
8.2.4.4. Kubandika kwenye
maeneo ya wazi / matangazo matokeo ya kura kwa kila mwombaji alivyopata baada ya Mkutano.
8.2.4.5.
Kuandaa Muhtasari wa Mkutano.
8.2.4.6. Kuwasilisha majina ya Wananchi
walioshinda pamoja na Muhtasari wa Mkutano kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za
Mitaa iliyopo kwenye Shehia husika.
9.0. MABARAZA YA KATIBA YA ASASI, TAASISI
NA MAKUNDI YA WATU
Kama ilivyoelezwa hapo awali, Kifungu cha 18 (6) cha Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, kinaeleza aina nyingine ya Mabaraza ya Katiba.
Tume inaruhusu Asasi, Taasisi au Makundi ya Watu wenye malengo yanayofanana kuandaa
mikutano kwa ajili ya kutoa fursa kwa wanachama wake kutoa maoni yao juu ya Rasimu
ya Katiba kisha kuwasilisha maoni hayo kwa Tume si zaidi ya tarehe 14 Agosti, 2013.
Mabaraza
hayo yatajiendesha yenyewe na kuwasilisha maoni yao kwa Katibu wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba. Orodha ya Mabaraza hayo ni pamoja na: 1.1. Jumuiya ya kidini. 1.2.
Chama cha siasa. 1.3. Asasi ya kiraia. 1.4. Taasisi ya elimu
ya juu. 1.5. Chama cha wafanyakazi. 1.6. Chama cha wakulima. 1.7.
Chama cha wafugaji. 1.8. Chama cha Wanahabari. 1.9. Mabaraza
ya Watoto, Taasisi za Kitaaluma, Vijana na Wazee. 1.10. Kundi au makundi ya
watu wenye malengo yanayofanana kama Sheria inavyoelekeza. 1.11. Kundi au makundi
ya watu wenye mahitaji maalum katika jamii.
10.0. TAREHE YA KUANZA
KUTUMIKA Mwongozo huu utaanza kutumika kuanzia tarehe 01 Machi, 2013.
Joseph
S. Warioba Mwenyekiti Tume ya Mabadiliko ya Katiba