2013-02-27 12:07:04

Kulipenda Kanisa kuna maanisha pia kuwa na ujasiri wa kufanya maamuzi magumu, yanayotesa, daima kwa ajili ya mafao ya Kanisa bila ya mtu kujitafuta mwenyewe!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Katekesi yake ya mwisho kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, siku ya Jumatano tarehe 27 Februari 2013 amewashukuru waamini, mahujaji na wageni waliomiminika kwa wingi mjini Vatican kusikiliza Katekesi yake.

Anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake ambayo imeweza kumkirimia katika kipindi chote cha utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu anasema, anasikia wajibu wa kuwashukuru wote aliokutana nao katika hija ya maisha yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa sababu hiyo haachi kufanya maombi na dua kwa ajili yao, ili wajazwe maarifa ya mapenzi ya Mungu katika hekima yote na ufahamu wa rohoni. Anawasihi kuenenda kama wajibu wao kwa Bwana, wakimpendeza kabisa, kwa kuzaa matunda kwa kila kazi njema na kuzidi katika maarifa ya Mungu.

Baba Mtakatifu anasema ana imani kubwa na maneno juu ya ukweli wa Injili ambao ni nguvu na maisha ya Kanisa; Injili inasafisha na kuuhisha na hatimaye, kuzaa matunda kwa wale wanaosikiliza kwa makini na kuipokea neema ya Mungu katika ukweli na upendo. Hii ndiyo imani na furaha inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa kipindi chote cha miaka minane ya uongozi wake.

Kwa imani aliweza kujiaminisha kwa Kristo na Kanisa lake, licha ya kutambua kwamba, dhamana hii ilikuwa ni kubwa hata pengine kuliko uwezo wake. Amebahatika kupata fursa za kufurahia maisha na kuona mwanga angavu; lakini amekutana pia na nyakati za giza, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro. Kanisa lilikumbwa na mawimbi mazito, kiasi cha kufikiri kwamba, pengine Yesu alikuwa amesinzia!

Lakini, aliendelea kutambua kwamba, ndani ya Mashua hii, yaani Kanisa, alikuwamo Kristo anayeliongoza na kamwe hawezi kuliacha kuzama! Yeye ni Nahodha na leo hii anasema Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwamba, daima ameliwezesha Kanisa pamoja na Papa mwenyewe kufarijika; kwa kuona mwanga na kuonja upendo wake.

Baba Mtakatifu katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani anawaalika waamini kujiaminisha zaidi kwa Kristo kama watoto wachanga mikononi mwa wazazi wao! Wajisikie kwamba, wanapendwa na Mungu kwani amemtoa Mwanaye wa Pekee ili kuwaonesha ule upendo usiokuwa na kifani. Kila mwamini asikie ile furaha ya kuwa Mkristo na kuendelea kufurahia zawadi ya imani, tunu kubwa ambayo hakuna mtu anayeweza kuwanyang'anya.

Mwenyezi Mungu anawapenda waja wake na kuwachangamotisha kupendana wao kwa wao pia! Baba Mtakatifu anawashukuru wote walioshiriki pamoja naye katika utekelezaji wa dhamana ya kuliongoza Kanisa la Kristo; watu ambao pengine wanatekeleza majukumu yao katika hali ya ukimya, kwa majitoleo na sadaka kubwa inayofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu.

Anawashukuru waamini wa Jimbo la Roma, Makleri, Watawa na Familia ya Mungu kwa ujumla. Wamemwonesha na akawaonjesha pia upendo wa kichungaji, unaofumbatwa katika utume wa kila kiongozi. Amemkumbatia kila mwamini katika sala, akionesha ule moyo wa kibaba! Anawashukuru watu wote kila mtu kwa nafasi yake, lakini kwa namna ya pekee, Mabalozi na wawakilishi wa nchi na watu wao mjini Vatican na wadau katika njia za mawasiliano ya Jamii, wanaotafuta mafao ya wengi!

Baba Mtakatifu anawashukuru watu wote walioungana naye kwa njia ya sala, kwani ametambua kwa dhati kabisa kwa hakika Papa si Mpweke! Amepokea barua na nyaraka nyingi kutoka kwa wakuu wa Serikali, Dini na Madhehebu mbali mbali, lakini pia ameendelea kupokea barua kutoka kwa watu wa kawaida kabisa wanaoonesha lile Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa linalofumbata: ukweli, upendo na furaha.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anakiri kwamba, katika miezi ya hivi karibuni, amehisi kwamba, nguvu zake zilikuwa zinaendelea kupungua; akasali kwa bidii kumwomba Mwenyezi Mungu, ili ampatie mwanga utakaomwezesha kufanya maamuzi makini, si kwa ajili ya mafao yake binafsi, bali kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa la Kristo. Ni uamuzi ambao ameufanya kwa kutambua uzito na upya wake, lakini katika utulivu wa ndani. Kulipenda Kanisa kuna maanisha pia kuwa na ujasiri wa kufanya maamuzi magumu, yanayotesa, daima kwa ajili ya mafao ya Kanisa bila ya mtu kujitafuta mwenyewe!

Baba Mtakatifu anasema, tangu tarehe 19 Aprili 2005 alijitoa kimaso maso kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, akitambua kwamba, hakuwa na jambo la pekee, kwani alikuwa amechaguliwa kwa ajili ya wote na kwa Kanisa zima! Ametambua kwamba, wale wanaompenda Kristo wanampenda pia Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anaonja umoja na mshikamano kutoka kwa waamini waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu kwa uhakika anasema, si kwamba, kwa sasa anarudia maisha ya utawala binafsi, kwa kutembea na kukutana na watu pamoja na kutoa miadhara. Si kwamba, anaukimbia Msalaba, bali sasa anajishikamanisha zaidi na Kristo Mteswa! Hana tena mamlaka ya utawala wa Kanisa, lakini bado anaendelea kubaki katika huduma kwa njia ya sala akiwa kwenye Viunga vya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Mtakatifu Benedikto atakuwa ni kielelezo na mfano mkuu wa kuigwa katika awamu hii mpya ya maisha yake, kama ushuhuda wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anawashukuru wote walioupokea na kuutambua uamuzi wake huu muhimu. Anasema kwamba, ataendelea kulisindikiza Kanisa katika hija yake kwa njia ya Sala na Tafakari hadi hatima ya maisha yake. Anawaomba kuendelea kumkumbuka katika sala mbele ya Mwenyezi Mungu, lakini zaidi kwa kusali kwa ajili ya kuwaombea Makardinali watakaohusika katika mchakato wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, mwishoni anasema, Mwenyezi Mungu ndiye anayeliongoza na kulienzi Kanisa lake nyakati zote: wakati wa raha na wakati wa shida. Huu ndio mwono wa hija ya imani kwa Kanisa na Ulimwengu. Yesu Kristo yuko daima pamoja na wafuasi wake na wala hatawaacha kamwe kwani anawakumbatia katika upendo wake mkamilifu.







All the contents on this site are copyrighted ©.