Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita baada ya kung'atuka rasmi madarakani hapo
tarehe 28 Februari 2013, saa 2:00 Usiku ataanza kuitwa "Baba Mtakatifu Mstaafu". Ufafanuzi
huu umetolewa na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican baada ya wanasheria
wa Kanisa kukaa na kulitafakari tukio hili la kihistoria katika maisha na utume wa
Kanisa.
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro tayari umesheheni waamini,
mahujaji na watu wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliofika kutoka
heshima zao za mwisho kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kama Khalifa wa
Mtakatifu Petro.
Ratiba inaonesha kwamba, Alhamisi, tarehe 28 Februari 2013,
Majira ya asubuhi, Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na Makardinali ambao wamekwisha
wasili hapa mjini Roma kwa ajili ya mazungumzo ya faragha. Jioni ataagwa rasmi na
Vikosi vya Ulinzi na Usalama mjini Vatican. Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu
wa Vatican ataongoza ujumbe wa viongozi waandamizi kutoka Vatican watakaomuaga Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kabla ya kuondoka rasmi mjini Vatican kuelekea
kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma.
Baba Mtakatifu
anatarajiwa kufika jioni mjini Castel Gandolfo, na huko atapokelewa na Kardinali Giuseppe
Bertello, Gavana wa Mji wa Vatican pamoja na Askofu mkuu Giuseppe Sciacca, katibu
mkuu wa Gavana wa Vatican, Askofu Marcello Semeraro wa Jimbo la Albano pamoja na viongozi
wa Serikali. Atakapo wasili Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, Baba Mtakatifu atatokeza
dirishani kusalimiana na wananchi pamoja na wageni watakaokuwa wamefika mjini Albano.
Saa 2:00 Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, atakuwa anang'atuka rasmi kutoka
madarakani na tangu wakati huo Kiti cha Ukulu wa Mtakatifu Petro kitakuwa wazi.
Walinzi
wa kutoka kutoka Uswiss ambao wamepewa dhamana maalum ya kumlinda Khalifa wa Mtakatifu
Petro, kadiri ya Mapokeo ya Kanisa, watakuwa wamemaliza utume wao na kurudi makao
makuu ya Vikosi hivi mjini Vatican. Vikosi vya ulinzi na usalama kutoka Vatican vitaendelea
kushughulikia masuala ya ulinzi na usalama wa Papa mstaafu. Tangu wakati huo, Baba
Mtakatifu hatavaa tena ile "Pete ya Mvuvi" inayoonesha ukulu wake kama Khalifa wa
Mtakatifu Petro wala hata vaa tena vile viatu vyekundu alama ya ushuhuda wa imani
hata ikibidi kumwaga damu!
Padre Lombardi anasema kwamba, mwanzo mwa Mwezi
Machi, Dekano wa Makardinali, atatuma barua ya mwaliko kwa Makardinali wote ili kushiriki
katika Mkutano wa Dekania ya Makardinali utakaokuwa na dhamana ya kuanza mchakato
wa uchaguzi wa Papa Mpya. Mikutano ya Makardinali inatarajiwa pia kuanza Juma lijalo.
Mikutano hii itafanyika kwenye Ukumbi Mpya wa Sinodi.
Kutokana na sababu za
kiufundi, Padre Lombardi anasema, Makardinali watahamia kwenye Hosteli ya Mtakatifu
Martha iliyoko mjini Vatican, siku moja kabla ya uchaguzi wa Papa Mpya. Utaratibu
wote utapangwa wakati wa mkutano wa Makardinali. Kikanisa cha Sistina ambacho kina
utajiri mkubwa wa Sanaa kitafungwa rasmi kuanzia tarehe 28 Februari 2013 ili kutoa
nafasi kwa ajili ya maandalizi ya mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya.