2013-02-27 11:34:52

Askofu Damian Dallu: Kwa hakika! Baba Mtakatifu Benedikto XVI analitajirisha Kanisa katika hija yake kuelekea utimilifu!


Uamuzi wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kung'atuka kutoka madarakani kunapania kwa namna ya pekee kabisa kulitajirisha Kanisa katika mchakato wa hija ya maisha yake kuelekea katika ukamilifu. Ni kiongozi ambaye amefungua lango kuu la historia ya Kanisa baada ya kupita takribani miaka 600 tangu tukio kama hili lilipotokea ndani ya Kanisa. RealAudioMP3

Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni la Kristo ataendelea kulipatia Kiongozi mwingine kadiri ya alama za nyakati. Kwa miaka minane, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ametekeleza yale aliyopaswa kutenda kadiri ya Mpango wa Mungu. Ni uamuzi ambao ameufanya baada ya kusali na kufanya tafakari ya kina na hatimaye, amelipatia Kanisa na Ulimwengu kwa ujumla wake, jibu makini kwamba, kwa sasa anag'atuka kutoka madarakani.

Ni uamuzi unaopaswa kupokelewa kwa jicho la imani, matumaini na mapendo, mintarafu Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Huu ni utambuzi wa Askofu Damian Dallu wa Jimbo Katoliki Geita, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican, wakati huu, Mama Kanisa anapomwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa uamuzi wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kung'atuka kutoka madarakani. Uamuzi alioufanya kwa utashi na uhuru kamili. Hiki kiwe ni kipindi cha kuimarika katika fadhila za kimungu yaani: imani, matumaini na mapendo.

Askofu Dallu anasema, sasa watu wamepata mang'amuzi kwamba, inawezekana katika mambo yale ambayo wengi hawakuyafahamu. Hii imekuwa ni changamoto ya kufanya tafiti zaidi kuhusu maisha ya kiroho, kichungaji na katika mahusiano na makuzi mazima ya ya historia ya wokovu. Ni kipindi cha kushukuru na kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kulipatia Kanisa mchungaji mkuu kadiri ya mapenzi yake!

Na kwa njia ya maombezi ya Roho Mtakatifu ambao ndio msingi wa imani ya Kanisa, waweze kufikia matumaini ya kweli, imani na upendo. Watu wengi wavutwe kwa Kristo, ili kumpenda, kumfuasa, kumtumikia na hatimaye wapate wokovu na uzima wa milele.







All the contents on this site are copyrighted ©.