Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, anawaalika waamini na
watu wote wenye mapenzi mema, kujitokeza kwa wingi katika Katekesi ya Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, inayotarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la
Mtakatifu Petro mjini Vatican, jumatano tarehe 27 Februari 2013, majira ya saa 4:30
asubuhi kwa saa za Ulaya. Hili litakuwa ni tukio la mwisho kwa Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita kuonekana hadharani kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Lengo
la Jimbo kuu la Roma, ni kumshukuru kwa utume ambao amelitendea Jimbo la Roma kama
Askofu wake katika kipindi cha miaka minane ya uongozi uliotukuka. Pale alipopata
nafasi ya kutembelea Parokia, aliwalisha waamini wake kwa Neno la faraja anasema Kardinali
Vallini. Amewawezesha waamini hao kuonja unyenyekevu, hekina na busara; amani na utulivu
wa ndani kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.
Huu ni wakati
wa kusali kwa ajili pamoja na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ili kumwombea
kwa Kristo mchungaji mkuu wa Kanisa lake. Kutokana na idadi kubwa ya waamini na watu
wenye mapenzi mema kutaka kushiriki katika tukio hili, Kardinali Vallini anasema kwamba,
watu hawatalazimika kuwa na tiketi za kuingia kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro, tiketi ni nguvu zako mwenyewe.
Kardinali Vallini anaendelea kuwahimiza
waamini kusali kwa ajili ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, pamoja na kuendelea
kuwaombea Makardinali watakaoshiriki katika mkutano wa kumchagua Papa mpya, ili waweze
kutekeleza wajibu huu tete kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa kwa sasa na kwa
siku zijazo!