2013-02-26 09:12:15

Serikali ya Malawi yapandisha kiwango cha mshahara wa kima cha chini kwa 61%


Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, inaipongeza Serikali kwa kusikia kilio cha wanyonge kiasi cha kuamua kupandisha mshahara wa kima cha chini kwa asilimia 61% na kima cha juu kwa asilimia 5%. Mwanzoni wafanyakazi walikuwa wanadai nyongeza ya asilimia 67% ya mshahara wa kima cha chini, lakini baada ya majadiliano ya kina na Serikali ya Malawi uamuzi ukafikiwa.

Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi inasema, kwamba, gharama ya maisha nchini Malawi imepanda kiasi kwamba hali ya maisha inazidi kushuka siku hadi siku, lakini wanaoathirika zaidi ni watu wa kawaida ambao wanaunda asilimia 80% ya wananchi wote wa Malawi. Inasikitisha kuona kwamba, ni asilimia 20% ya wananchi wa Malawi wanaoendelea kufaidi matunda ya uhuru jambo ambalo halikubaliki katika mchakato wa kudumisha misingi ya haki jamii.

Hivi karibuni, Serikali ya Malawi iliamua kushusha thamani ya fedha yake hali ambayo ilipelekea kupanda kwa gharama ya bidhaa na huduma nchini humo na watu wengi wakajikuta kwamba, hawana uwezo wa kununua bidhaa na huduma zilizokuwa zinatolewa sokoni. Ni kundi dogo la wananchi wa Malawi wanaoweza kumudu gharama za huduma ya afya pamoja na kuwasomesha watoto wao katika shule binafsi.







All the contents on this site are copyrighted ©.