Sadaka ya Ijumaa kuu ijenge na kuimarisha mshikamano wa kiimani na Wakristo wanaoishi
katika Nchi Takatifu
Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki limewaandikia Barua Mabalozi wa Vatican
sehemu mbali mbali za dunia kuhimiza mchango wa waamini unaotolewa wakati wa Ijumaa
kuu, kama kielelezo cha mshikamano wa dhati na waamini wanaoishi katika Nchi Takatifu.
Hawa ni wale ambao wamebaki na wanaendelea kutunza maeneo matakatifu, kwani walibahatika
kupata urithi wa imani. Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, tukio hili la mshikamano
lipewe msukumo wa pekee na Makanisa mahalia. Kipindi cha Kwaresima, kiwe ni sehemu
ya maandalizi kwa ajili ya kuchangia kwa ukarimu na upendo kwa wale wanaoishi katika
Nchi Takatifu, kwa hali na mali. Waamini wahamasishwe kushiriki katika tendo hili
ambalo limekuwa likipewa msukumo wa pekee na Viongozi wa Kanisa. Ni mchango unaopania
anasema Kardinali Leonardo Sandri kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu katika Nchi
Takatifu na kwenye Makanisa yaliyoko Mashariki.