Makardinali kuamua tarehe ya uchaguzi wa Papa mpya!
Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican, akizungumza na waandishi wa habari
mjini Vatican, siku ya Jumatatu tarehe 25 Februari, 2013 anabainisha kwamba, mkutano
wa Dekania ya Makardinali wenye dhamana ya kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro katika
kikao chake cha kwanza, utataja tarehe maalum ya kufanya uchaguzi wa Papa mpya. Ili
kuwa na uhakika wa tarehe rasmi ya uchaguzi wa Papa, kuna haja kwa waamini na watu
wote wenye mapenzi mema, kuendelea kuvuta subira hadi tarehe za mwanzo mwanzo za Mwezi
Machi, 2013.
Makardinali wenye dhamana ya kupiga na kupigiwa kura wanapaswa
kushiriki katika mkutano wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro. Lakini pia wanaweza
kutohudhuria mkutano huu kwa sababu mbali mbali kama vile ugonjwa. Kwa Kardinali ambaye
anaamua kwa utashi wake mwenyewe kutohudhuria mkutano, hataruhusiwa tena kushiriki
katika mkutano huo hata kama atakuwa amebadilisha uamuzi wake.
Wataalam wa
sheria za Kanisa bado wanaendelea kukuna vichwa ili kutafuta jina ambalo Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita ataitwa mara baada ya kung’atuka rasmi kutoka madarakani;
jina ambalo litaendelea kuonesha heshima na dhamana aliyokuwa nayo kama Khalifa wa
Mtakatifu Petro. Papa ndiye mwenye dhamana ya kutomruhusu Kardinali yoyote yule kuingia
na kushiriki mkutano wa Makardinali, pale inapoonekana kwamba, inafaa na kwa ajili
ya mafao ya Kanisa.
Wakati wote wa mikutano ya Makardinali kama njia ya kufahamiana,
kutathmini na kupembua hali ya Kanisa, changamoto na matarajio ya Watu wa Mungu, Makardinali
hawataruhusiwa kuhojiwa wala kuzungumza na Waandishi wa Habari wakati wote wa mikutano
yao kwani wanafungwa na siri ya mchakato mzima wa uchaguzi wa Papa Mpya.
Dekano
wa Makardinali ambaye kwa sasa ni Kardinali Angelo Sodano ataamua tarehe na muda kwa
Makardinali kuweza kukutana na kuendesha mikutano yao. Ndiye pia mwenye dhamana ya
kufahamu ni Makardinali wangapi ambao wako tayari mjini Roma na wanaweza kuhudhuria
mkutano wa Dekania ya Makardinali na wale ambao bado hawajawasili.