2013-02-26 08:10:02

Mabadiliko katika kanuni na sheria wakati wa uchaguzi wa Papa


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita ameamua kwa utashi wake mwenyewe kufanya mabadiliko katika Waraka wa Kichungaji unaojulikana kama Universi Dominici Gregis unaoshughulikia uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Itakumbukwa kwamba, kunako tarehe 21 Juni 2007 Waraka huu ulibainisha kwamba yule atakayechaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, atatakiwa kupata theluthi tatu ya kura zote zitakazokuwa zimepigwa.

Ili kufanikisha zoezi hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita ameamua katika waraka wa sasa kufafanua baadhi ya vipengele vilivyokuwa vimekwisha bainishwa kwenye Waraka wa Universi Dominici Gregis.

Mambo msingi yaliyoibuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa sasa ni kwamba, Kadiri ya Waraka uliopita, mkutano wa Makardinali kwa ajili ya kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro ulipaswa kufanyika kati ya siku 15 hadi 20 tangu pale Kiti cha Khalifa wa Mtakatifu Petro kinapokuwa wazi. Kwa sasa Baba Mtakatifu anasema, mkutano unaweza kuanza mapema ikiwa kama Makardinali wanaohusika wako tayari mjini Vatican. Lakini huu ni uamuzi unaopaswa kufanywa na Makardinali wenyewe.

Baba Mtakatifu anatumia neno “walau” ili uchaguzi uweze kuwa halali idadi ya kura zitakazopigwa na Makardinali wenye dhamana ya kuchagua inapaswa kuwa ni theluthi tatu au zaidi. Kwa Kardinali yeyote atakayetoa siri ya uchaguzi wa Papa atakuwa amejitenga moja kwa moja na Kanisa. Adhabu hii kwa lugha ya Kilatini inajulikana kama “Latae Sententiae”. Hapa Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa Makardinali kutunza siri ya uchaguzi wa Papa! Sheria ya zamani ilikuwa inatoa ruhusa kwa Papa Mpya kumchukulia hatua za nidhamu Kardinali atakayevunja siri ya uchaguzi wa Papa.

Kifungo cha siri ya uchaguzi kinawabana hata wataaalam watakaokuwa wameshirikishwa katika mkutano wa kumchagua Papa Mpya. Siri hii inapaswa kutunzwa ndani ya Kikanisa na Nje ya Kikanisa cha Sistina.

Katika uamuzi wake, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amefanya pia mabadiliko yafuatayo ambayo kimsingi hayana uzito mkubwa kuliko hayo ambayo tayari yamekwisha fafanuliwa. Sheria ya awali ilikuwa inasema kwamba, Makardinali wote wangepelekwa kwenye Kikanisa cha Sistina kwa usafiri maalum na kwamba, wakati wakielekea kwenye mkutano wa uchaguzi wa Papa hawaruhusiwi kuzungumza na mtu!
Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, wakati wote wanapokuwa wakielekea kwenye mkutano kwa kutumia usafiri au kwa miguu hawataruhusiwa kuzungumza na watu njiani.

Baba Mtakatifu ameongeza idadi ya washereheshaji wa mkutano wa Makardinali kutoka wawili hadi nane kutokana na kuongezeka kwa idadi ya Makardinali wanaoshiriki katika kupiga kura ya kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kutakuwepo na Maandamano makubwa kutoka Kikanisa cha Mtakatifu Paulo hadi kwenye Kikanisa cha Sistina mahali unapofanyikia uchaguzi wa Papa.

Kuna mabadiliko kidogo pia katika utendaji wa shughuli za Camerlengo msaidizi. Kwa sasa hata Makardinali ambao hawana tena dhamana ya kupiga au kupigiwa kura watashiriki katika Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kuombea uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kabla ya uamuzi huu wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Makardinali waliovuka umri wa miaka themanini tangu walipozaliwa walikuwa hawaruhusiwi kushiriki hata kwenye Ibada ya Misa Takatifu. Ibada hii itaongozwa na Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali ingawa yeye hana tena dhamana ya kupiga au kupigiwa kura kutokana na umri wake.








All the contents on this site are copyrighted ©.