Bado Kristo anawatuma Wafuasi wake kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa ushuhuda wa
maisha yao!
Hapo mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa Mungu. Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu.
Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea, wale waliomwamini
aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu. Hakuna mtu aliyemwona Mungu kamwe. Mwana wa
pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba ndiye aliyetujulisha habari za
Mungu.
Wakati Yohane Mbatizaji alipokuwa anabatiza watu mtoni Yordani, wafuasi
wawili wa Yohane Mbatizaji yaani Andrea na Nduguye Simoni Petro walimsikia akisema
kuwa Yesu ndiye Mwana Kondoo wa Mungu wakaamua kuacha yote na kumfuata, kwani walitambua
kwamba, wamekutana na Masiha, yaani Kristo.
Wafuasi wengi wa Yesu kama vile
akina Andrea na Filipo walitoa ushuhuda wao juu ya utimilifu wa Unabii na Sheria kama
ilivyobainishwa kwenye Maandiko Matakatifu. Itakumbukwa kwamba, Yesu kadiri ya Injili
ya Luka, siku moja, Yesu alikuwa amesimama kando ya Ziwa Genesareti, akiwa amezungukwa
na watu wengi, wakisikiliza Neno la Mungu, akaingia katika mashua ya moja iliyokuwa
ya Simoni akamtaka aisogeze majini, mbali kidogo na ukingo wa ziwa. Akaketi, akafundisha
umati wa watu akiwa ndani ya mashua.
Siku moja katika pita pita zake, Yesu
alimwona mtoza ushuru kwa jina Lawi, akamwambia nifuate, akaacha yote akaamua kumfuata
na kumwandalia Yesu karamu kubwa, akakaa pamoja na watoza ushuru, jambo ambalo lilipelekea
Mafarisayo kuanza kunung’unika kwa kuwa alikua anakula na wadhambi pamoja na watoza
ushuru. Lakini Yesu aliwajibu kwamba, wenye afya hawamhitaji tabibu bali wagonjwa
ndio wenye shida kubwa, akawaambia kwamba, hakuja kuwaita wenye haki bali wadhambi
ili watubu na kuongoka.
Wote hawa wameitwa kwa nyakati tofauti kutoka katika
medani mbali mbali za maisha na utume wao, lakini wanatumwa kutangaza Habari Njema
ya Wokovu. Tafakari hii ya Neno la Mungu iwasaidie waamini kuendelea kulitafakari
Fumbo la Kanisa lililoanzishwa na Yesu, wakati huu, watu wengi wanapoendelea kumsindikiza
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa sala na sadaka yao kutokana na uamuzi
wake wa kung’atuka kutoka madarakani.