Wanazuoni wanaomboleza kifo cha Kardinali Julien Ries, bingwa wa elimu ya binadamu
mintarafu maisha ya kiroho!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika salam zake za rambi rambi kutokana
na kifo cha Kardinali Julien Ries kwa Askofu Guy Harpigny wa Jimbo Katoliki la Tournai,
Ubelgiji anasema, amepokea habari za msiba huu kwa masikitiko makubwa.
Anamwombea
Marehemu kardinali Ries ili Mwenyezi Mungu aweze kumwangazia mwanga wa milele mja
wake katika imani, aliyelihudumia Kanisa kwa mafundisho na tafiti zake mintarafu historia
ya dini; sehemu ambayo alionesha umahiri mkubwa. Kardinali Ries ametolea ushuhuda
wa imani yake kwa kukazia moyo wa majadiliano.
Kardinali Julien Ries, Jaalim
mstaafu wa historia ya dini Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Louvain, Ubelgiji, tarehe
23 Februari 2013 amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 93. Alizaliwa tarehe 14 Aprili
1920. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi akapadrishwa kunako tarehe 12 Agosti
1945. Katika maisha yake alijikita zaidi katika tafiti za kisayansi kiasi kwamba,
wanazuoni wengi walimtambua kuwa ni kati ya waasisi uelewa wa binadamu mintarafu maisha
yake ya kiroho.
Alikuwa ni mwandishi mahiri, hadi anaitupa mkono dunia alikwisha
andika vitabu 650 vilivyotafsiriwa katika lugha kumi na moja za kimataifa. Kwa miaka
mingi alifundisha katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Lovanio. Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita, akamteua kuwa Kardinali kunako mwaka 2012 kwa kutambua mchango wake
mkubwa katika tafiti za kisayansi.