2013-02-25 08:35:49

Uamuzi wa Papa Benedikto XVI kung'atuka madarakani hauna budi kuheshimiwa!


Kung’atuka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kutoka madarakani kumepokelewa kwa hisia mbalimbali na mshangao mkubwa. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili yake na kwa ajili ya Kanisa, daima wakitumainia neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Basi tumsindikize Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI kwa moyo wa shukrani na sala kwa tendo huru, ambalo amelitekeleza kutoka katika dhamiri nyofu, mintarafu mwanga wa Injili. Ameamua jambo hili, kwa kutambua udhaifu wake na mipaka inayotokana na “umri wake mkubwa” kiasi cha kumfanya kushindwa kutekeleza utume wake kwa ukamilifu zaidi katika jamii inayokumbwa na mabadiliko makubwa na changamoto mbalimbali.
Ni maneno yaliyosikika kutoka kwa baadhi ya watu waliohojiwa na Radio Vatican kwa nyakati mbali mbali. Wanasema “Tupokee uamuzi huu katika jicho la imani kuwa ni fundisho la maisha ya kiroho linalofungua lango la Kanisa katika safari ya maisha. Tunapofikiria uamuzi wake huo katika Mlango wa Imani tunaweza kutambua kwamba, kung’atuka kwake ni kielelezo ch abusara na usomaji wa “alama za nyakati” na mwaliko wa neema ya Mungu kwa ajili ya ujenzi wa udugu, umoja, upendo na mshikamano kwa kuweka kando matamanio ya kidunia ili kushirikiana na Yesu Kristo katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu.
Kristo ni mfano bora huduma kama alivyoonesha siku ile ya Alhamisi Kuu, alipowaosha mitume wake miguu. Tuendelee kusali na kutafakari kwa tujikabidhi mikononi mwa Roho Mtakatifu anayeendelea kutenda maajabu yake katika maisha yetu ya kila siku.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema, anapanda Mlimani ili kusali na kutafakari zaidi na wala si kulikimbia Kanisa. Ni maneno yenye unyenyekevu wa hali ya juu, ambayo baadhi ya vyombo vya habari vimeshindwa kuyazingatia kwa kutoa shutuma zisizo na msingi kwamba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anakimbia matatizo na changamoto zinazolikabili Kanisa.
Jumapili iliyopita maelfu ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia walifika mjini Vatican kumsindikiza Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa sala pamoja na kumuaga kwa majitoleo yake makuu kwa Kanisa la Kristo kwa kipindi cha miaka minane. Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro ulikuwa umefurika na kuwacha watu wengi wameshikwa na mshangao mkuu!








All the contents on this site are copyrighted ©.