2013-02-25 07:44:46

SECAM: Utawala bora, mafao ya wengi na demokrasia katika kipindi cha mpito!


Heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu, ndiyo kauli inayobeba barua ya kichungaji kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM inayochambua kwa kina na mapana juu ya utawala bora, mafao ya wengi na demokrasia katika kipindi cha mpito.

Hii ni barua inayoelekezwa kwa watu wote wenye mapenzi mema barani Afrika. SECAM inaamini kwamba, kila mtu pamoja na Kanisa wana wajibu wa kutafuta mafao ya wengi, kusimama kidete kulinda na kujenga Jamii inayosimikwa katika misingi ya haki na amani. Kanisa daima limeendelea kufanya hija na watu katika furaha, majonzi na matumaini yao.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema Uinjilishaji upanie kurithisha tunu msingi za Kiinjili, ili waamini waweze kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, changamoto iliyotolewa na Mababa wa awamu ya pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika, katika mchakato wa kudumisha haki, amani na upatanisho miongoni mwa Jamii.

Lengo la barua hii ya kichungaji iliyotolewa na SECAM na kutiwa sahihi na Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa SECAM inasema, lengo ni kuonesha mchango wa Kanisa katika harakati za kuhamasisha utawala bora na demokrasia katika kipindi cha mpito Barani Afrika. Kanisa halifungamani na chama chochote cha kisiasa, bali linataka kuonesha na kushirikisha tunu msingi zitakazosaidia mchakato wa kutafuta na kudumisha haki, uhuru, utu na heshima kwa binadamu. Tunu hizi ni muhimu katika kuunda na kukuza Jamii yenye amani na utulivu.

Kanisa linatambua kwamba lina dhamana ya kuwa ni sauti ya kinabii; chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa. Katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, Kanisa Barani Afrika limesimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu sanjari na kujita katika kudumisha maendeleo endelevu ya binadamu mintarafu dhana ya upatanisho, haki na amani.

Kanisa limeendelea kuwa ni sauti ya wanyonge wanaohitaji huruma, sadaka na uchaji wa Mungu. Hawa ni waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi, wajane na watoto yatima. SECAM imeendelea kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, kwa kujikita zaidi na zaidi katika kuhamasisha mafao ya wengi na utawala bora; tunu msingi katika kudumisha amani na demokrasia katika kipindi cha mpito. Lengo la kuhimiza tunu msingi za maisha ya Kiinjili ni kuhakikisha kwamba, watu wa Afrika wanapata utimilifu wa maisha.

Ili kuweza kutekeleza dhamana hii kuna haja kwa Bara la Afrika kuwa na viongozi wanaojitoa kimaso maso kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wao. Huu ndio mchango ambao umeendelea kutolewa na Mabaraza ya Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Afrika katika mchakato wa kipindi cha mpito kuelekea katika demokrasia ya kweli na amani dumifu. Baadhi ya Maaskofu wamekuwa ni wanachama wa tume za upatanisho Barani Afrika. Kanisa limetekeleza wajibu na dhamana yake katika masuala ya kisiasa na kuonesha msimamo thabiti katika masuala ya rasilimali na utajiri wan chi husika, ili uweze kutumika kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.

SECAM inasema kwamba, kumekuwepo na maendeleo ya kuridhisha katika mchakato unaopania kujenga misingi ya utawala bora; hali ya maisha ya watu kwa kiasi fulani imeendelea kuboreka na kwamba, juhudi za mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi zinaonesha mafanikiio ingawa bado kuna mengi yanayopaswa kutekelezwa katika matumizi bora ya rasilimali ya nchi; mapambo dhidi ya umaskini, ubadhirifu na ufisadi wa mali ya umma kwa kushirikiana na makampuni pamoja na wawekezaji wasio waaminifu ndani na nje ya Bara la Afrika.

Hata baada ya kuadhimisha Jubilee ya miaka 50 ya uhuru wa bendera, uchumi wa nchi nyingi Barani Afrika bado ni duni na kwamba, kuna baadhi ya viongozi wanaoendelea kujinufaisha wenyewe kinyume kabisa cha mafao ya wengi. Bado vita, kinzani na migogoro ya kisiasa, kijamii na kidini inaendelea kufuka moshi sehemu mbali mbali za Bara la Afrika, kiasi cha kutishia amani na utulivu pamoja na kuendelea kusababisha ongezeko la wimbi kubwa la watu wasiokuwa na makazi maalum. Vijana wengi Barani Afrika hawana fursa za ajira na kwamba, kuna haja ya kuwekeza zaidi kwa wanawake ili waweze kutekeleza wajibu wao ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

SECAM inabainisha kwamba, mwishoni mwa miaka ya 1980, dhana ya utawala bora ilikuwa ni kama ndoto ya kufikirika. Hata hivyo, bado majadiliano kati ya Serikali na wadau mbali mbali wa maendeleo ni hafifu kwa nchi nyingi za Kiafrika, hususan katika vikao vinavyofanya maamuzi muhimu. Hii ni kutokana pia na uhasama wa kisiasa uliopo kati ya wananchi.

Mababa wa awamu ya pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika, walitoa changamoto kwa wanasiasa kukoleza tunu msingi za kiinjili katika mchakato wa mabadiliko ya kisiasa kwa kujikita katika uaminifu, ushirikishwaji, uvumilivu pamoja na ari ya kutaka kuhudumia badala ya kuhudumiwa, jambo ambalo Baba Mtakatifu anasema, linahitaji toba na wongofu wa ndani. Kuna haja ya kuendeleza dhana ya ukweli na uwazi; tija na uaminifu ili kujenga na kuimarisha Jamii inayotafuta mafao ya wengi.

Viongozi Barani Afrika hawana budi kubadilika: kitabia na kimwono, kwani dhana ya utawala bora inafumbata pia maadili yanayopania mafao ya wengi yanayopatikana katika masuala ya: kijamii, kisiasa, kiuchumi na kitamaduni. Kila mwananchi anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na kwamba, upendeleo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Ukosefu wa haki unaofanywa na baadhi ya watu ndani ya Jamii ni jambo ambalo haliwezi kukubalika hata kidogo! Kila mtu anapaswa kupewa haki yake.

Mafao ya wengi yanahimiza mabadiliko ya tabia kwa kujikita katika upendo na haki, kwa ajili ya mafao ya Jamii nzima. Sera na mikakati ya kiuchumi haina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Watu wapate mahitaji yao msingi na kwamba, wote wanahimizwa kutafuta mafao ya wengi katika masuala ya huduma, mazingira, afya, maarifa, habari, amani na usalama.

Kwa maneno mengine, Jamii inahimizwa kutumia vyema rasilimali ya nchi kwa mafao ya wengi, kwa sasa na kwa ajili ya kizazi kijacho. SECAM inawachangamotisha viongozi Barani Afrika kujenga umoja na mshikamano kwa kuondokana na tabia ya ubaguzi wa raia wao na badala yake kudumisha majadiliano ili kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa, iili haki na usawa viweze kutawala ndani ya Jamii. Watu wasaidiwe kwa hali na mali ili kuweza kushiriki katika maendeleo ya Bara la Afrika kadiri ya uwezo wao, wakiongozwa na ukweli wa Kiinjili.

SECAM katika barua yake ya kichungaji kwa watu wenye mapenzi mema Barani Afrika inasikitika kusema kwamba, rushwa imekuwa ni saratani inayoendelea kudhohofisha: mfumo wa uchumi, utawala, soko la ajira, afya, elimu na mahakama. Nchi nyingi zimelitambua tatizo hili na kwamba, kuna baadhi ya Serikali zimeanza kulivalia njuga ili kulitokomeza, lakini juhudi hizi zinagonga mwamba kutokana na ubinafsi, kiasi cha kusahau mafao ya wengi. Kwa hakika, SECAM inasema, kuna haja kwa Jamii kuhakikisha kwamba, haki inatawala kwa kujikita katika: utu na maadili mema; ukweli na uaminifu; mambo yanayopaswa kujidhihirisha katika maisha ya kila siku.

SECAM inabainisha kwamba, kumekuwepo na kipindi cha mpito katika demokrasia kutoka utawala wa chama kimoja cha siasa hadi utawala wa vyama vingi vya kisiasa na kwamba, uchaguzi ni jukwaa linalopembua maamuzi ya viongozi watakaoshika madaraka ndani ya Jamii. Hapa panapaswa kuwa ni mahali pa majadiliano yanayojengeka katika msingi wa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti, ili kujenga na kuimarisha amani na utulivu.

Kanisa linatambua mchango mkubwa unaoweza kutolewa na chaguzi huru na haki katika ujenzi wa nchi na demokrasia. Hapa ni mahali ambapo pamepelekea maafa makubwa katika nchi kadhaa za Kiafrika. Kanisa kwa upande wake, linapaswa kuendeleza majadiliano, uhamasishaji wa wananchi wengi kushiriki zaidi na kuanzisha mchakato wa upatanisho pale kinzani na misigano inapojitokeza.

Viongozi wachaguliwe na wawajibishwe na wananchi wao, kwani demokrasia ni kwa ajili na pamoja na watu! Kumekuwepo na mabadiliko makubwa kutoka utawala wa chama kimoja cha kisiasa hadi utawala wa vyama vingi vya kisiasa, lakini chaguzi nyingi Barani Afrika zimegeuka kuwa ni uwanja wa fujo na kinzani za kivita! Hii ni kutokana na ubinafsi, uchu na uroho wa mali na madaraka kwa baadhi ya viongozi Barani Afrika. Hata hivyo kuna mabadiliko makubwa Barani Afrika kwani nchi nyingi zilizokuwa zinachechemea kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe sasa cheche za amani na utulivu zinaanza kuonekana walau kwa mbali, ingawa hali bado ni tete nchini Mali na Nigeria pamoja na baadhi ya nchi za Kiafrika ambamo vurugu za kidini zinaonekana kushika kasi kubwa!

SECAM inasema kuwa mchakato wa kipindi cha mpito kuelekea demokrasia hauna budi kujengeka katika misingi ya: uhuru, ukweli, uwazi katika zoezi zima la chaguzi za kisiasa, kwa kuzingatia pia kanuni na sheria za demokrasia. Kukosekana kwa demokrasia ya kweli kumepelekea uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu. Hizi ni dalili za baadhi ya viongozi kukosa uzalendo. Umefika wakati kwa Bara la Afrika kuona ni aina gani ya mfumo wa utawala unaoweza kuwa ni bora zaidi kwa ajili ya mafao ya wengi, kwa kuzingatia maana halisi ya demokrasia na mafao ya wengi.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM katika barua yake ya kichungaji linaendelea kusema kwamba, Bara la Afrika liko mikononi mwa Waafrika wenyewe! Vyama vya kiraia, viongozi wa Bara la Afrika, wananchi na watu wenye mapenzi mema kwa Bara la Afrika wanapaswa kuungana na kushikamana kwa dhati kwa ajili ya mwanzo mpya! Watu wajikite katika kudumisha utawala bora, kuthamini na kuenzi mafao ya wengi na mchakato wa mabadiliko ya kidemokrasia Barani Afrika.

Wawe mstari wa mbele kulinda na kutetea haki msingi za binadamu. Vitoe elimu ya uraia ili watu wengi zaidi waweze kushiriki katika vikao vya maamuzi ya maisha yao. Watu wajishughulishe kuzuia migogoro na kinzani, kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano badala ya kukimbilia kwenye mtutu wa bunduki kama suluhu ya migogoro na kinzani Barani Afrika. Watu watafute mafao ya wengi na kamwe wasikubali kuwa ni vibaraka wa wanasiasa wanaotaka kuwatumia kwa ajili ya mafao yao binafsi.

Bara la afrika lina utajiri na rasilimali kubwa ya watu na maliasili, lakini kwa bahati mbaya wananchi wake bado wanaogelea katika umaskini, vita, kinzani na migogoro ya kila aina, mambo ambayo kwa nadra sana yanasababishwa na majanga asili ana badale yake ni maamuzi tenge na vitendo vya kibinadamu dhidi ya mafao ya wengi. SECAM inawahamasisha viongozi wa Bara la Afrika kujifunga kibwebwe kupambana na umaskini kwa kutumia rasilimali na utajiri unaopatikana Barani Afrika. Kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi pamoja na kuhakikisha kwamba, chaguzi zinafanyika katika mazingira huru, ukweli, uwazi na amani, daima kwa kutafuta mafao ya wengi.

Bara la Afrika lijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano katika medani mbali mbali za maisha, kwa kukuza na kuimarisha demokrasia na haki msingi za binadamu na kwamba, taasisi za Umoja wa Afrika zishughulikie kikamilifu changamoto za watu wa Afrika. Ni mwaliko wa kuondokana na ubaguzi wa kisiasa, kidini na kikabila, kila mwananchi apewe fursa ya kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Jamii yake. Familia ya Mungu na Taasisi mbali mbali za Kanisa Barani Afrika zisaidie kubaini mizizi ya ukosefu wa haki: kitaifa na kimataifa pamoja na vita.

Waamini wajikite pia katika majiundo endelevu na ushuhuda ili wawe ni vyombo vya demokrasia, haki za binadam na utawala bora. Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake: Dhamana ya Afrika; Africae Munus. Wakristo wawe ni mashahidi wa Uinjilishaji wa kina, daima wakijitahidi kumwilisha utawala bora. Waamini wajitahidi kuyafahamu Mafundisho Jamii ya Kanisa ya kuyamwilisha katika medani mbali mbali kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Itifaki mbali mbali zilizoridhiwa na nchi za Kiafrika kuhusu demokrasia, chaguzi na utawala bora zitekelezwe kwa umakini mkubwa. Kanisa liendelee kuhimiza haki, amani, ukweli na uwazi.

Kila mtu atekeleze wajibu wake, kwa kuchuchumilia toba na wongofu wa ndani ili kujenga na kudumisha Jamii iliyo bora zaidi sanjari na ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaojielekeza zaidi katika: haki, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ufalme wa Mungu unasimikwa katika ukweli, umoja, msamaha, uvumilivu, huduma, maadili, mshikamano, matumizi sahihi ya vyombo vya mawasiliano ya Jamii, amani na utunzaji bora wa kazi ya uumbaji. Umefika wakati wa Bara la Afrika kusimama na kutembea kifua mbele!

Barua ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar iliyotiwa mkwaju na Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa SECAM ni changamoto chanya inayopaswa kufanyiwa kazi Barani Afrika ili kujenga na kuimarisha utawala bora, mafao ya wengi na kipindi cha mpito kuelekea demokrasia ya kweli.

Imehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.