Kwaresima ni kipindi cha toba, matendo ya huruma na utii kwa maagizo ya Mwenyezi Mungu
Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro katika mahojiano maalum na Radio
Vatican anawaalika waamini wakati huu wa Kipindi cha Kwaresima sanjari na Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kuanza hija ya maisha
mapya, kwa kumtii Mwenyezi Mungu. Anasema, Imani
bila matendo hiyo imekufa ndani mwake! Kumbe, kuna haja kwa waamini kumwilisha imani
yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya matendo ya huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii, kila mtu akijitahidi kuwa kweli ni Msamaria mwema kwa jirani
yake. Ni mwaliko wa kuwa na mwono mpana zaidi kwa kuwaangalia wote wanateseka kutokana
na majanga asilia, vita na madhulumu. Kwaresima kiwe ni kipindi cha maandalizi
ya kina katika Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.
Kwaresima iwawezeshe waamini kujenga fadhila ya imani, matumaini na mapendo katika
Fumbo la Ufufuko wa Kristo, ili hatimaye, kuweza kulitolea ushuhuda. Askofu Mkude
anasema kwamba, Imani ya Wakristo wa mwanzo ilijikita katika Ufufuko, wakaliona Kaburi
wazi, hapo ukawa ni mwanzo wa Habari Njema ya Wokovu inayojikita katika: maisha, maneno
na matendo ya Yesu Kristo kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu kutoka katika lindi la
dhambi na mauti.