2013-02-23 07:43:05

Wagombea Urais nchini Kenya wapinga utamaduni wa kifo!


Marais watarajiwa kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Kenya hapo tarehe 4 Machi 2013 wameonesha msimamo wao wa kupinga vitendo vya utoaji mimba pamoja na ndoa za watu wa jinsia moja nchini Kenya. Hayo yamebainishwa wakati wa madahalo ulioendeshwa na vyombo vya habari nchini Kenya, kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu nchini humo.

Baadhi ya viongozi waliohojiwa wanasema kwamba, wanapenda kukumbatia utamaduni wa kuenzi zawadi ya maisha, dhidi ya utamaduni wa kifo. Wanasema, Katiba ya Kenya imefafanua vyema maana ya ndoa kuwa ni uhusiano kati ya watu wa jinsia mbili tofauti, kumbe hapa hakuna mjadala, kwani viongozi watakaochaguliwa watakuwa na jukumu la kulinda na kutetea Katiba ya nchi ambayo kimsingi ni sheria mama.

Umefika wakati kwa wananchi kuongozwa na dhamiri nyofu badala ya kufuata mkumbo kwa tamaduni za kigeni zinazoonesha kukengeuka kwa misingi ya maadili na utu wema. Utoaji mimba ni mauaji na kwamba, hakuna mtu mwenye mamlaka ya kukatisha uhai wa jirani yake.

Hii ni kazi ya Mwenyezi Mungu aliyemuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake ndiye pia mwenye dhamana ya kuchukua uhai wa kiumbe chake kadiri ya mapenzi yake mwenyewe. katika mdahalo huo, baadhi ya viongozi wanaogombea urais nchini Kenya hawakuonesha msimamo wao wa wazi dhidi ya utoaji mimba na ndoa za watu wa jinsia moja, ambao kwa baadhi ya nchi wahisani zimekuwa ni vigezo vya kupata misaada.







All the contents on this site are copyrighted ©.