Rais Giorgio Napolitano aagana na Papa Benedikto XVI mjini Vatican
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumamosi tarehe 23 Februari 2013 baada ya
kutoka kwenye Mafungo ya kiroho, amekutana na kuzungumza na Rais Giorgio Napolitano
pamoja na ujumbe wake mjini Vatican. Mazungumzo ya viongozi hawa wawili yalikuwa ni
mazito na yenye kuonesha urafiki wa dhati baina ya viongozi hawa ambao wamefahamiana
na kushirikiana kwa muda mrefu.
Rais Napolitano amemshukuru Baba Mtakatifu
kwa niaba ya wananchi wa Italia kwa uwepo wake wa karibu katika nyakati mbali mbali.
Wanatambua na kuthamini mchango na mafundisho ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita katika masuala ya kidini na kimaadili, wanaahidi kwamba, wataendelea kumsindikiza
katika maisha yake kwa njia ya sala.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita,
kwa upande wake, amemshukuru sana Rais Giorgio Napolitano pamoja na mkewe kwa urafiki
wao na kuitakia Italia ufanisi mkubwa kwa ajili ya mafao ya wengi, hasa wakati huu
Italia inapofanya uchaguzi mkuu wa viongozi wake, dhamana fungamanishi.