2013-02-23 09:27:48

Msimamo wa Maaskofu wa IMBISA


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA, hivi karibuni limekutana na kufanya mazungumzo na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, kama ambavyo pia waliwahi kuzungumza naye kabla ya mkutano wao mkuu uliofanyika kunako mwaka 2001 na mwaka 2004.

Maaskofu wa IMBISA wanapongeza hali ya mshikamano na umoja wa kitaifa inayoendelea kujionesha kama kielelezo cha matumaini mapya katika mchakato wa kufufua uchumi na kujikita katika maendeleo ya wananchi wa Zimbabwe. Maaskofu wanasema, Kanisa linaunga mkono demokrasia ya kweli, umuhimu wa kulinda na kuheshimu Katiba ya nchi ambayo ni sheria mama; haki za binadamu na umuhimu wa kila raia kutekeleza wajibu na dhamana yake ndani ya Jamii husika.

Kanisa linapania kusimama kidete kutetea: haki, mafao ya wengi, uchaguzi huru na wa haki pamoja na kushirikiana kwa karibu zaidi na tume ya uchaguzi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi. Maaskofu wa IMBISA wanaendelea kuonesha mshikamano wao na wananchi, katika zile nchi ambazo zinajiandaa kwa ajili ya kufanya uchaguzi mkuu kwa mwaka 2013.

Wanawaalika waamini, wananchi na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, chaguzi zinazingatia: amani, uhuru, ukweli na uwazi. Kusiwepo na madhulumu ya kisiasa bali kila Chama cha kisiasa kizingatie na kuheshimu Katiba ya nchi ambayo inatakiwa kupigiwa kura ya maoni na wananchi wa Zimbabwe.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa ihakikishe kwamba, hata wapinzani wanapata nafasi ya kutumia vyombo vya mawasiliano ya Jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Serikali.







All the contents on this site are copyrighted ©.