2013-02-23 08:02:22

Mauaji ya kinyama yanaendelea kuitikisa Syria!


Askofu mkuu Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Syria anasema, anasikitishwa sana na mashambulizi yanayoendelea kufanyika nchini Syria na yanayolenga kuharibu miundo mbinu kama vile: majengo ya Makao makuu ya Wizara ya Fedha, Elimu na Benki kuu, licha ya maelfu ya watu wasiokuwa na hatia wanaoendelea kupoteza maisha yao siku hadi siku. Mji mkuu wa Damasco umejaa maiti kiasi kwamba, hali hii kwa sasa limekuwa ni jambo la kawaida.

Askofu mkuu Zenari anasema kwamba, kuna zaidi ya watu 70, 000 ambao wamepoteza maisha yao tangu vita ya wenyewe kwa wenyewe ilipozuka nchini Syria. Jumuiya ya Kimataifa bado inaendelea kulifumbia macho tatizo hili wakati ambapo athari za vita hii zinaendelea kujionesha kwa kasi kubwa. Kuhusu uvumi kwamba, kuna mpango wa kutaka kushambulia Ubalozi wa Vatican nchini Syria, Askofu Mkuu Zenari anasema hana uhakika na ukweli wa habari hizi.

Jambo la msingi ni kwa Jumuiya ya Kimataifa kuingilia kati ili kuweza kukomesha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yanayoendelea kufanyika nchini Syria. Vita haina macho wanaoteseka na kuuwawa ni wananchi wa Syria na wala risasi au bomu linapopigwa halichagui wala kubagua dini au imani ya mtu!







All the contents on this site are copyrighted ©.