Jopo la Marais wastaafu kushughulikia mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi
Waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa nchini Malawi Bwana Patrick
Kabambe amesema kwamba, mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi unatarajiwa kusuluhishwa
na viongozi wakuu watatu kutoka Afrika. Viongozi hao ni: Rais mstaafu Joachim Chisano
wa Msumbiji, Rais mstaafu Thabo Mbeki wa Afrika ya Kusini na Rais mstaafu Festus Mogae
wa Botswana.
Viongozi wa Malawi na Tanzania tayari wamekwisha wasilisha hoja
na misimamo ya nchi zao kuhusu mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi. Jopo la
Marais wastaafu kutoka Afrika linatarajia kuanza kutekeleza kazi yake mwishoni mwa
mwezi Februari, 2013. Mgogoro huu ulishika kasi na kuingia katika medani za kimataifa
pale Malawi ilipotoa idhini kwa kampuni moja ya kimataifa kuanza kuchimba mafuta kwenye
Ziwa Nyasa kwa madai kwamba, Ziwa lote ni mali yao.