2013-02-23 14:26:44

Hatima ya Mashua ya Mtakatifu Petro iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu!


Sekretarieti ya Vatican inapenda kusisitiza kwamba, Dekania ya Makardinali inafuata sheria na kanuni zinazoongoza katika mchakato wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro. Huu ndio msimamo ambao umekuwa ukichukuliwa na Vatican kwa nyakati zote na kwamba, uchaguzi wa kiongozi mkuu wa Kanisa ni kwa ajili ya mafao ya Kanisa na wala si vinginevyo!

Kwa karne mbali mbali, Makardinali walijikuta wakikabiliana na mashinikizo yanayotolewa dhidi ya Kardinali mmoja mmoja au Dekania nzima ya Makardinali, lengo likiwa ni kuingilia kati maamuzi na hatimaye, kuipigia dunia magoti kwa mitazo ya kisiasa na kidunia. Kulikuwepo na nguvu za dola kutoka kwa baadhi ya nchi ambazo zilidhani kwamba, zinaweza kuingilia dhamana ya uchaguzi wa Papa, mchezo huu mchafu umejitokeza tena wakati huu. Ni mambo ambayo yanapewa kipaumbele bila kuzingatia maisha ya kiroho pamoja na kusoma alama za nyakati kwa maisha na utume wa Kanisa kwa sasa!

Sekretarieti kuu ya Vatican inabainisha kwamba, wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Makardinali watapaswa kuchunguza dhamiri zao mbele ya Mwenyezi Mungu na kutoa maamuzi yao kwa utashi na uhuru kamili. Inasikitisha kuona kwamba, kuna mafuriko ya habari za uvumi yanayoendelea kutolewa na vyombo vya habari yenye lengo na nia ya kuwachafua baadhi ya Makardinali na taasisi husika.

Wakati huu, pengine kuliko wakati mwingine wowote, Waamini wa Kanisa Katoliki wanapenda kuzingatia yale mambo msingi: kusali kwa ajili ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita; wanamwomba Roho Mtakatifu ili awaangazie Makardinali watakapokuwa wanatekeleza dhamana yao ya kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, wanasali kwa ajili ya kumwombea Papa mpya atakayechaguliwa, kwa kutambua kwamba, hatima ya Mashua ya Mtakatifu Petro iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.