2013-02-23 08:48:01

Dhamana ya Kanisa katika mchakato wa maendeleo endelevu Sudan ya Kusini


Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Sudan ya kusini ni hatua kubwa katika mikakati ya maendeleo endelevu nchini Sudan ya Kusini, ambayo hivi karibuni imekuwa ni nchi huru ya 54 Barani Afrika. Itakumbukwa kwamba, baada ya kura ya maoni, kunako tarehe 9 Julai 2011 Sudan ya Kusini likawa ni taifa huru.

Kanisa kwa miaka mingi limekuwa ni mdau mkubwa wa maendeleo na mtetezi wa haki msingi za binadamu, kumbe uhusiano wa kidiplomasia na Vatican wanasema Maaskofu wa Sudan ni hatua ya kutambua mchango wa Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Sudan katika ujumla wao.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya alitumwa kuwakilisha ujumbe wa Vatican kwenye Maadhimisho ya Uhuru wa Sudan ya Kusini. Wananchi na waamini katika ujumla wao, walionesha nia ya kutaka kushirikiana kwa karibu zaidi na Vatican. Sudan ya Kusini inakadiriwa kuwa na Waamini wa Kanisa Katoliki millioni nane.

Sudan ya Kusini ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 39 duniani, kumbe Vatican inakuwa ni nchi 40 kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Sudan ya Kusini. Nchi 16 tayari zimekwisha fungulia ofisi za balozi zake mjini Juba na Sudan ya Kusini imekwisha fungua balozi 13 nchi za nje. Itifaki ya uhusiano huu wa kidiplomasia kati ya Vatican na Sudan ya Kusini ni matokeo ya majadiliano ya kina kati ya Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, ingawa hata Askofu mkuu Leo Boccardi anaendelea pia kutekeleza majukumu yake ya kidiplomasia hata kwa Sudan ya Kusini.

Uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande hizi mbili unalenga kulihamasisha Kanisa Katoliki kuwekeza zaidi likiwa na uhakika wa rasilimali yake katika mikakati ya maisha ya kiroho, kichungaji sanjari na maendeleo endelevu yanayoweza kuchangiwa pia na Jumuiya ya Kimataifa. Sudan ya Kusini inapania pamoja na mambo mengine kutafuta ufumbuzi wa matatizo na vikwazo ambavyo vimekuwa vikikwamisha sera na mikakati ya maendeleo kwa watu wake, kwa kuwekeza zaidi katika misingi ya haki, amani na utulivu.

Kwa njia hii, Sudan ya Kusini itaweza kuwa na uhuru zaidi kwa watu kutoka sehemu moja hadi nyingine wakitafuta fursa za ajira, makazi na maendeleo binafsi. Wananchi wa Sudan wanataka kuwa na uhakika wa usalama wa mali na maisha yao na kamwe hawataki tena kuendelea kuishi katika hali ya vitisho vya kutimuliwa kutoka Sudan Kongwe. Kardinali Zuber Wako, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Khartoum, hivi karibuni alisikika akisema kwamba, waamini Jimboni mwake wanaendelea kupungua.







All the contents on this site are copyrighted ©.