2013-02-22 07:16:53

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima


Mpendwa msikilizaji, ni Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka C wa Kanisa na Neno la Mungu latualika na kututaka kuwa watu wa sala kama Bwana anavyosali pale mlimani kama tusomavyo katika Injili ya Dominika hii.

Matokeo ya sala ya Bwana ni ufunuo wa ukuu wa Mungu kwa njia ya Mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo kwa wanadamu. Bwana anaposali anageuka na kung’ara na hivi kugeuka sura ni tokeo la msisitizo katika sala na muunganniko na Mungu. Mara moja bila kuchelewa kila awaye yote ambaye anataka kuungana na Mungu lazima ajikite katika maisha ya sala inayozama tumaini la kweli na unyenyekevu mkamilifu.

Sala ya Bwana wetu Yesu Kristo inatuingiza katika maisha ya Kwaresima ambacho ni kipindi cha kupanda kinachodai kuingia ndani ya maisha yetu na hivi kuweza kuchokonoa kugeuka sura yaani kugeuka mioyo yetu na kuunganika na Bwana. Mwinjili Luka anasisitiza maisha ya Sala akitaka kutuambaia kuwa kipindi cha kwaresima kinapata nguvu maana iliyo sahihi katika maisha ya kuongea na Mungu. Kumbe mkristu ambaye anajiibidisha kushika vema safari ya kwaresima anapaswa kutambua kuwa Kugeuka sura ya maisha yake kunawezekana tu chini ya mwanga wa maisha ya sala.

Ni kutoka kwa Mungu tu nguvu ya kuweza kutembea kuelekea maisha mapya, maisha ya pasaka yaweza kupatikana. Kwa njia ya sala Bwana anatenda mapenzi ya Mungu, anakamilisha kazi ya ukombozi wetu kwa njia ya msalaba ambao anaubeba na kuvumilia kwa sababu ya muunganiko wake na Baba yake.

Katika kugeuka sura kwa Bwana, Mitume walipata furaha na hata wakaona waombe kubaki palepale mlimani, hili mara moja latufundisha kuwa kukutana na Bwana na hasa katika kipindi cha kwaresima kwatuletea furaha na matumaini. Hata hivyo, Mitume wanaposikia habari yakuwa Bwana atakufa wanapata usingizi, na watafanya vivyohivyo kule Getsemane. Hii ni dalili ya kutoelewa kinachotokea kwa Bwana, ni dalili ya woga wa mateso ambayo Bwana atayapokea.

Sisi leo tuko upande gani? Naona wakati fulani tunakuwa katika usingizi, hatuoni mateso ya Bwana kama mateso ya kuteletea wokovu na pia tunashindwa kuyatazama mateso ya maskini na wenye shida mbalimbali kama njia ya kushiriki mateso ya Bwana.

Mpendwa msikilizaji, pale mlimani, Mitume wanapata furaha na toka na furaha waliyoipata wanamwomba Bwana kujenga vibanda vitatu ili waweze kubaki palepale! Hii ni dalili ya kuchoka na kutotaka kuendelea na safari ya Bwana ambayo itaishia msalabani. Hivi leo nasi twaweza kupata furaha katika Misa Takatifu na tukatamani kubaki kanisani, wakati mwaliko wa Misa yaani, “missio” ni kwenda na kuingia katika mitaa na jumuiya zetu na zaidi kwa mataifa kwa ajili ya kutangaza habari njema ya wokovu ambayo tumeipokea katika Neno na Ekaristi Takatifu.

Katika kutangaza habari njema tunasindikizwa na nguvu ya sala kama barabara kuelekea huduma timilifu katika umisionari wetu. Maisha ya sala yanapaswa yawe ndiyo chakula chetu cha kila siku ili kwacho tunaweza kupata kuungana na Bwana mwezeshaji wa kazi nzima ya kitume.

Tunaendelea polepole mpendwa mwana wa Mungu kuona yanayomtokea Mwana wa Mungu, kunatanda wingu zito na jeupe likiwa ni dalili ya uwepo wa Mungu katika utume wa Bwana. Mitume wanaonjeshwa ulimwengu wa juu, ulimwengu mpya unaopatikana kwa sala na kufunga. Mara inatokea sauti toka mbinguni huyu ni mwanangu mpendwa msikieni yeye. Ni tafsiri ya Baba juu ya tendo la Yesu Kristo la kutimiza mapenzi yake, hakika Yesu Kristo ni mteule wa Mungu.

Sauti hii tuliisikia wakati wa ubatizo wa Bwana, Mungu akitangaza kuwa Huyu ni Mwanae Mpendwa, ni Mwana wa Mungu. Mpendwa katika hili unaalikwa kumsikiliza na kumsikia mteule wa Mungu na kumfuata mpaka anapomaliza kazi yake pale msalabani.

Jambo la kumsikia na kumsikiliza Mwana wa Mungu linaunganika na jambo la Bwana kubaki yeye peke yake wakati Musa na Elia wanatoweka. Manabii hawa wanawakilisha Agano la kale, yaani sheria na manabii na kutoweka kwao maana yake kazi yao imekamilika na sasa Bwana wetu Yesu Kristu ndiye mfalme wa Agano Jipya ndiye mkuu atakayeongoza historia na kumfikisha mwanadamu kufika mbinguni.

Sote twafahamu Manabii hawa wawili ni sura zenye nguvu katika Agano la Kale na hivi kuwepo kwao na kisha kutoweka kwaonesha nguvu ya Kristo juu yao na Agano la Kale. Kwa tendo hili tuna uhakika hakuna kiongozi mwingine tuliyepewa na Baba kwa ajili ya kutufikisha mbinguni isipokuwa Yesu Kristo tu.

Mpendwa msikilizaji, kumfuasa Bwana aliyegeuka sura, anayetuonjesha ufufuko wake, inatudai kuwa makini kama ambavyo Mt. Paulo anavyowafundisha Wafilipi. Anasema yatupasa kuepuka kuwa watu wa kuabudu tumbo, yaani kujali mambo binafsi na kushiriki mipango inayopingana na mapenzi ya Mungu. Wajibu sasa ni kujikatalia kwa njia ya sala na majitoleo yetu na kujenga urafiki mkamilifu na msalaba wa Bwana. Ulevi, uzululaji, uvivu, rushwa, ufisadi ni kinyume na msalaba wa Kristu, ni kinyume na kuishi kipindi cha kwaresima.

Kama tulivyokwisha dokeza tunaalikwa kutambua kuwa, Kwaresima ni kipindi cha kutafakari na kutubu, ni kipindi cha kutazama msalaba na kuchota nguvu na upendo na kisha kwenda kuhudumia wanaohangaika. Ni kipindi cha kupanda mlima pamoja na Bwana kwa njia ya sala na na matunda yatakuwa ni kung’ara sura zawadi ya inayotokana na mastahili ya ufufuko wa Bwana. Yafaa kuvuka giza la utumwa wa dhambi na kifo, tukisaidiwa na matumaini, tukisaidiwa na sakramenti na Neno la Mungu.

Yafaa katika Kipindi cha Kwaresima kusali kama Kardinali Newman aliyekuwa akisema “ Bwana, sikuombi nione mbali zaidi bali hatua fupi ambapo nitaweza kuweka nyayo zangu” Tunapaswa kuomba kuona kwa jicho la upendo wale ndugu zetu waliokaribu nasi. Hatuna haja ya kwenda mbali sana bali kutazama mateso ya Bwana pale tulipo na kuweza kutoa jibu ambalo angetoa Bwana. Kila ndani ya mmoja wetu kuna sura ya Bwana inayong’ara pale mlimani na hivi kuitazama kwa upendo hali tukingojea ufufuko wa Bwana.

Nakutakia furaha tele na furaha hiyo ikufanye ukamtumikie Bwana katika familia na mahali pote unapokuwa na hapo ndipo kuna kuishi kwaresima ya mwaka huu na juma hili. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya, C.PP.S.









All the contents on this site are copyrighted ©.