2013-02-21 13:54:30

"Udaku" kuhusu kung'atuka kwa Baba Mtakatifu Benedikto XVI


Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ataendelea kuitwa kwa jina hili ambalo amelitumia kwa kipindi chote cha miaka minane ya uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baada ya kung'atuka madarakani rasmi hapo tarehe 28 Februari 2013, saa 2:00 Usiku, ataitwa Askofu mstaafu wa Jimbo kuu la Roma, lakini bado wanasheria wa Kanisa wanaendelea kulitafakari kwa kina suala hili.

Pete ya Mtakatifu Petro ambayo amekuwa akiitumia kama kielelezo cha dhamana na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro inaweza kuvunjwa, kwani ni kielelezo cha ukuu wake wakati wa mawasiliano ya faragha. Papa anavishwa pete hii na Dekano wa Makardinali wakati wa kuanza utume wake ndani ya Kanisa. Pete hii ni alama ya ukuu wake kama Khalifa wa Mtakatifu. Wakati wa kifo, Kardinali Camerlengo anamvua na kuivunja pete hiyo mbele ya Makardinali kama alama ya kuhitimisha uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Padre Lombardi anasema kwamba, Waraka wa kitume ambao Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita alikuwa anajiandaa kuuandika kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, hataweza tena kuuchaapisha kutokana na muda uliosalia kwa upande wake kuwa madarakani. Ujumbe huu unaweza kutolewa kwa namna ya nyingine, lakini si kama Waraka wa kichungaji.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, mara baada ya kuondoka mjini Vatican, kuanzia tarehe 28 Februari 2013 ataishi kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma, hadi mwanzoni mwa Mwezi Mei. Baadaye atahamia kwenye Monasteri ya "Mater Ecclesiae" iliyoko mjini Vatican ambayo kwa sasa inafanyiwa ukarabati mkubwa, ulioanza tangu Novemba 2012 na unatarajiwa kukamilika hivi karibuni. Hapa ni mahali ambapo Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu mara mbili.

Wakati wote huu, Baba Mtakatifu ataendelea kusaidiwa na Askofu mkuu Georg Gaenswein, mkuu wa nyumba ya kipapa na ndiye atakayekuwa mhusika mkuu wa kutoa taarifa za Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita wakati wote huo. Hakuna taratibu wala ratiba ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuonekana hadharani tena baada ya kung'atuka kutoka madarakani hapo tarehe 28 Februari 2013.

Mkutano wa Dekania ya Makardinali wenye dhamana ya kumchagua Papa mpya, unaojulikana kama "Conclave" maana yake "kufungiwa na ufunguo" unatarajiwa kufanyika kati ya tarehe 15 hadi 20 Machi 2013, ili kutoa nafasi kwa Makardinali kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuweza kuwasili na hatimaye kushiriki katika tukio muhimu katika maisha na utume wa Kanisa. Kunaweza kutokea mabadiliko, ikiwa kama Makardinali wenye dhamana ya kupiga kura watakuwa tayari wamekwisha wasili mjini Roma.

Baba Mtakatifu anaendelea kutafakari kama kuna umuhimu wa kuandika mawazo yake binafsi kuhusu suala hili kwa siku za usoni. Padre Lombardi anawaalika wadadisi wa masuala ya Kanisa kuvuta subira, ili kutoa nafasi kwa Baba Mtakatifu kulifanyia kazi wazo hili! Makardinali 117 watashiriki katika mkutano wa kumchagua Papa mpya, kati yao Makardinali 67 ni wale walioteuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Kuanzia tarehe Mosi, Machi 2013, Makardinali wote watakaoshiriki katika uchaguzi wa Papa mpya watalazimika kuhamia mjini Vatican kwenye Hosteli ya "Domus Sanctae Marthae". Dekano wa Makardinali ni Kardinali Angelo Sodano. Lakini kwa vile amekwishavuka miaka 80 tangu alipozaliwa ataweza kushughulikia masuala yote ya uchaguzi nje ya Kikanisa cha Sistina. Wakati wa uchaguzi mhusika mkuu atakuwa ni Kardinali Giovanni Battista Re, dekano kadiri ya umri na kwamba, yeye ni Kardinali, Askofu. Kumbuka kwamba, kuna Makardinali, Mashemasi, Mapadre na Maaskofu, ndo Top!







All the contents on this site are copyrighted ©.