Mawazo ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuhusu: binadamu na utamaduni kuanzia mwaka
1972 hadi mwaka 2005 yamekusanywa katika kitabu kimoja
Mada kumi na nne zilizoandikwa na Kardinali Joseph Ratzinger kuanzia mwaka 1972 hadi
mwaka 2005 kabla ya kuteuliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu
Petro, zimekusanywa na kuchapishwa katika kitabu kimoja kinachojulikana kama "Joseph
Ratzinger in Communio: Anthrolopology and culture", na kuhaririwa na David L. Schindler
na wenzake.
Baadhi ya mada zinazojadiliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita ni: ubinadamu, dhana ya uzazi na kazi ya uumbaji; Yesu Kristo kwa nyakati
hizi; maana ya Siku ya Bwana; Fadhila ya Matumaini; teknolojia ya usalama inayojadiliwa
kwa jicho la kimaadili pamoja na dhana ya Mungu mintarafu Mafundisho ya Mwenyeheri
Yohane Paulo wa Pili.
Kitabu cha kwanza chenye mkusanyo wa mada zilizoandikwa
na Kardinali Joseph Ratzinger wakati huo kuhusu "Umoja wa Kanisa" kilichapishwa kunako
mwaka 2010. Lengo ni kuona mchango wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika
uelewa wa: Kanisa, binadamu na mabadiliko ya mwenendo wa taalimungu. Itakumbukwa kwamba,
Jarida la "Communio" lilianzishwa kunako mwaka 1972 na wanataalimungu mahiri kama
akina Hans Urs von Balthasar, Henri de Lubac, Jean Luc Marion na Joseph Ratzinger
mwenyewe.